Friday, March 22, 2024

MAHUNDI AZINDUA UCHIMBAJI WA VISIMA VYA MAJI KATA TANO WILAYA YA MBARALI

Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Mhandisi Maryprisca Mahundi amezindua mradi wa uchimbaji visima vya maji uzinduzi uliofanyika Kijiji cha Azimio Mapula Kata Kongolo Mswiswi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ambapo Kata tano zitanufaika na mradi huo Wilaya ya Mbarali.

Mahundi amesema Wizara itakamilisha kiasi cha shilingi milioni 96 hivi karibuni kwa lengo la kuukamilisha mradi huo ili mitambo iweze kuhamie Kata zingine nao waonje keki ya Mama Samia Suluhu Hassan. Naibu waziri amesema visima vingine vitachimbwa katika vijiji vya Mpolo, Iwalanje, lbohola, Limsemi, Nyakazombe na Vikaye.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbarali Mhandisi Samwel Heche amesema mpaka sasa visima ishirini vimechimbwa Mkoani Mbeya tangu kuwasili mtambo huo Mkoani Mbeya na mradi wa Azimio Mapula ukikamilika utagharimu  shilingi 107,352,742/- mpaka sasa zimetumika  shilingi  10,400,000/- ili mradi ukamilike zinatakiwa shilingi 96,952,742 hivyo ameiomba Wizara kukamilisha fedha hiyo kukamilisha mradi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbaral Kanali Denis Mwila mbali ya kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji na vyanzo vya amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mji,Naibu Waziri wa Maji kwa kutatua kero ya maji.

Aidha Diwani wa Kata ya Mswiswi Eliah Bange amemshukuru Naibu Waziri wa Maji kwa kutatua kero ya maji katika vitongoji vyote vitano vya Kata yake.


Bange ameitumia nafasi hiyo kuiomba RUWASA kuboresha baadhi ya miundo mbinu ya maji katika kata yake ambayo mingi imechakaa na ongezeko la watu limefanya maji kushindwa kutosheleza wakazi wa Kata ya Mswiswi.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Mbarali Zabibu Nuroo ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani.

Uzinduzi wa uchimbaji visima vya maji Wilaya ya Mbarali umeendana na maadhimisho ya wiki ya maji duniani yaliyoanza Machi 16, 2024 na kilele chake ni Machi 22, 2024.

No comments:

Post a Comment