Monday, March 11, 2024

TECNO YAPONGEZWA KWA KUBORESHA HUDUMA YA MAWASILIANO MBEYA

Serikali mkoani Mbeya imeipongeza kampuni ya kutengeneza simu za mkononi ya TECNO kwa kuendelea kuboresha mawasiliano na maisha ya watanzania na kuyataka makampuni mengine kuiga mfano huo ili kuongeza ushindani.

Hayo yamesemwa na Afisa Michezo Mkoa wa Mbeya Robert Mfugale akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera wakati wa uzinduzi wa duka la TECNO lililopo Soweto Jijini Mbeya.


"Niwapongeze TECNO kwa kuwa wabunifu na kuona umuhimu wa kuwekeza katika mkoa wetu wa Mbeya na kuweka duka kubwa ambalo litaleta mageuzi makubwa na teknolojia, hakuna ulimwengu unaoenda bila teknolojia sasa mtu anaweza kupata taarifa kiganjani kwake" amesema Mfugale.

Pia Mfugale ameyataka makampuni mengine kuiga mfano wa TECNO ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kuongeza ubora na ubunifu wa bidhaa zinazoendana na mahitaji ya jamii kwa wakati husika.

Naye Meneja wa TECNO Mkoa wa Mbeya Jerome William amesema kampuni hiyo imejipanga kufungua maduka mengine katika mkoa wa Mbeya ili kusogeza huduma kwa wananchi sambamba na kutoa ajira kwa vijana.

"Nia ya kwanza ni kuiunga mkono serikali katika uwekezaji wa viwanda, pia kutengeneza ajira kwa vijana, na mwisho ni kusogeza huduma kwa jamii ili wananchi wapate simu janja karibu na maeneo yao badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma zetu" amesema William.

No comments:

Post a Comment