Monday, June 29, 2026

RIPOTI MAALUM: KUTOKA MOTO WA KUFUKUZA FISI HADI MWANGA WA UMEME

 Umeme wageuza vijiji kuwa vituo vya maendeleo; shule, biashara na kilimo vyanufaika…

Na Sanula Athanas aliyekuwa Shinyanga

 


Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Masunula, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wakisoma TEHAMA kwa vitendo katika moja ya madarasa ya shule hiyo hivi karibuni. Sekta ya elimu imenufaika na ujio wa umeme vijijini. PICHA: SANULA ATHANAS

KIJIJI cha Masunula katika Kata ya Usule, Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, kina historia inayofanana na mamia ya vijiji vingine nchini.

Kilianzishwa mwaka 1974 kupitia Operesheni Vijiji (1973-1976), mkakati wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, uliolenga kuwakusanya wananchi katika maeneo maalum ili kurahisisha utoaji huduma za msingi kama elimu, afya, maji na miundombinu mingine ya maendeleo.

Kwa miongo mitano, wakazi wa Masunula waliishi maisha ya kawaida ya vijijini yaliyotawaliwa na matumizi ya mafuta ya taa kwa mwanga, mashine zinazotumia dizeli kwa shughuli za uzalishaji na uhaba wa huduma nyingi za kisasa zilizokuwa zikionekana kama haki ya wakazi wa mijini pekee.

RIPOTI MAALUM: JINSI TANZANIA INAVYOJINASUA KUTOKA UTEGEMEZI WA MAFUTA

Vituo 50 vya kuchaji magari ya umeme kusimikwa katika mikoa yote nchini, serikali yapanga kununua magari ya umeme na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia

 

Na Sanula Athanas aliyekuwa Dodoma 

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, akiwa pamoja na viongozi wengine, akiweka jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa kituo cha kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) jijini Dodoma, Juni 11 mwaka huu. PICHA: SANULA ATHANAS

 

KILA siku, Juma Mwinuka (29) huamka alfajiri na kuanza kazi yake ya kubeba abiria kwa bajaj katika eneo la Kimara Golani, jijini Dar es Salaam.

Kwa miaka mingi alikuwa akitumia bajaj inayotumia petroli, jambo lililomlazimu kutumia kati ya Sh. 20,000 na 25,000 kwa siku kununua mafuta.

Lakini leo maisha yake yamebadilika. Akiwa ameketi katika bajaj yake ya umeme, Mwinuka anasema ameshuhudia tofauti kubwa kati ya teknolojia ya zamani na mpya. 

“Nilikuwa natumia Sh. 20,000 hadi 25,000 kwa siku kununua petroli. Sasa nachaji bajaj yangu kwa gharama isiyozidi Sh. 8,000 kwa siku,” anasema huku akitabasamu.