Monday, March 25, 2024

TULIA TRUST YATOA MIFUKO 400 YA SARUJI KUSAIDIA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

Taasisi ya Tulia Trust imechangia mifuko ya saruji 400 kwa Shule za Sekondari Dk Tulia Girls, Itende  sambamba na Shule ya msingi Mlimani iliyopo Kata ya Sinde Jijini Mbeya.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo amekabidhi mifuko hiyo leo na kuweka wazi ni utekelezaji wa ahadi ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo na Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini, Dkt. Tulia Ackson.

Mwakanolo ameagiza uongozi wa Shule hizo kusimamia kikamilifu saruji iliyotolewa itumike kwa malengo yaliyokusudiwa kuchochea sekta ya elimu.

Amechanganua kuwa kwa Shule ya Msingi Mlimani imetolewa mifuko ya saruji 200 wakati Sekondari ya Itende 100, huku Shule ya Sekondari Dkt. Tulia Girls mifuko 100.

Amesema lengo ni kuona wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ya kujifunzia na kufanya vyema kwenye masomo ili kutimiza ndoto zao na kuja kuwa chachu kwa taifa na watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi mlimani, Jane Mwaisumo ameshukuru kwa mchango huo na kwamba utasaidia kuboresha miundombinu ya matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Fanuel Fyanua amesema katika Kata zote za Jiji la Mbeya yeye amependelewa kwa kupewa idadi kubwa yaa mifuko ya saruji na sababu kubwa ni changamoto ya hali ya miundombinu.

“Kuna changamoto kubwa ya miundombinu ya matundu ya vyoo vyumba vya madarasa tunamshukuru sana Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwa mchango wake mkubwa kwenye sekta ya elimu".

Ofisa Elimu Msingi Kata ya Sinde Onoratha George amesema shule hiyo ina changamoto kubwa ya mrundika wa wanafunzi na kuomba Serikali kuunga mkono juhudi za Mbunge Dkt. Tulia Ackson kutatua changamoto hizo.

No comments:

Post a Comment