Wednesday, March 20, 2024

MADIWANI MBEYA WAVUTIWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI

Madiwani viti maalum Jiji la Mbeya wamesema wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Maji iliyosimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBEYA - UWSA).

Kauli hizo wametoa Jumanne Machi 19, mwaka huu baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi wa Ilungu Wilaya ya Mbeya vijijini uliogharimu Sh 4.8 bilioni na mradi wa Itagano na Mwansekwa yenye thamani ya Sh 5.2 bilioni.

Diwani viti maalum Attu Msai na Mjumbe wa bodi ya Maji mesema miradi hiyo imekuwa mkombozi mkubwa  kwa wananchi kwani walikuwa na  adha kubwa kwa kipindi kirefu.

“Ni matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kwa kazi nzuri zinazofanywa kutatua changamoto moto mbalimbali za wananchi” amesema Msai.

Msai amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wanajivunia kwa kasi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali na kuhaidi kura za kishindo katika chaguzi zijazo ikiwepo wa Serikali za mitaa na Mkuu 2025.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji, Mhandisi Barnabas Konga amesema katika kuadhimisha wiki ya Maji na miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan wamefanya mambo kadhaa ikiwepo kutembelea mradi wa chanzo cha Mto Kiwira ambao utagharimu Sh 250 bilioni na kuzalisha lita milioni 117 kwa siku.

“Mradi wa Mto Kiwira uko katika hatua nzuri za  usanifu na ujenzi ambao ikikamilika utakuwa  mwarobaini wa kuondoa tatizo la Maji kwa mji wa Mbalizi na Mkoa wa Mbeya kwani utakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 1.4 milioni kwa siku” amesema Konga.

Konga amewataka Madiwani kutumia fursa za uwepo wa mradi huo kushawisha wananchi kusogezewa huduma ili kuwezesha mamlaka kufikia malengo iliyojiweka  kufikisha Maji safi na salama mpaka sasa watu 700 wamechukua fomu huku 30 wamefikishiwa huduma.

“Leo tumefanya ziara nanyi waheshiwa Madiwani viti maalum lengo ni kuwaonyesha uwekezeji wa Serikali katika miradi ya Maji kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu ikiwa ni matunda ya kujivunia  kwa watanzania” amesema Konga.

Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Neema Stanton amesema kila mwaka wanafanya maadhimisho ya wiki ya Maji kuanzia Machi 16 mpaka 22 na kufanya mambo mbalimbali sambamba na kutoa elimu kwa jamii kutunza vyanzo vya maji kwa kuacha shughuli za kilimo ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

“Miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan tumefanya ziara na Madiwani Viti maalum lengo ni wakaisaidie serikali kukemea  wananchi kuachana na vitendo vya kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo ili kulinda rasilimali za nchi" amesema Stanton.

Pamoja na mambo mengine, Stanton amesema watafanya shughuli mbalimbali ikiwepo zoezi la kusafisha vyanzo vya Maji na kupanda miti na kuhamasisha jamii utunzaji mazingira.

No comments:

Post a Comment