Wednesday, March 20, 2024

AFISA TARAFA AKERWA NA WATENDAJI WAZEMBE

Afisa Tarafa ya Ilongo Magdalena Sikwese ameagiza Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha wanatumia nafasi zao kwa kuwatumikia Wananchi vizuri ikiwemo kuwa na kauli nzuri, kuwa wakarimu, kusoma mapato kwa wananchi, kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.


"Watendaji tumeshau wajibu wetu wa kusoma mapato na matumizi. Sisi Watendaji tumefika kwenye maeneo ya Wananchi tukajifanya nasisi wananchi, tumesahau kwamba hao Wananchi tumewafahamu baada ya kupata ajira hapo." 

Sikwese amesema unaposoma taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi inatia moyo hata utakapowaomba michango mingine ya kimaendeleo itakuwa rahisi kujitoa.
Pia Sikwese amesema kila mtu akitimiza wajibu wake ipasavyo, basi Tarafa ya Ilongo itakuwa na maendeleo huku akikemea tabia ya baadhi ya Watendaji kuwajibu vibaya Wananchi pale wanapohitaji huduma kutoka kwao.

Sikwese amewataka Watendaji kuacha tabia ya kukataa kuwasikiliza Wananchi hata kama wamefika muda wa kuchelewa kwakuwa Wananchi wanaamini Watendaji ndio jawabu la mwisho kuhusu shida zao na kutegemea msaada zaidi.

Kwa upande mwingine, baada ya Watendaji wa Kata na Maafisa Elimu kuwasilisha taarifa zao za utekelezaji wa maendeleo katika kata zao, idadi ya Watendaji wa vijiji waliohudhulia kikao hicho haikuwa ya kuridhisha na kupelekea Sikwese kutoa tamko la kuwaorodhesha Watendaji wote wa vijiji ambao hawajahudhulia.

 

Hata hivyo, aliwaomba Watendaji wa vijiji kuwasilisha taarifa zao za utekelezaji lakini chakushangaza wengi hawakuwa na taarifa za utekelezaji. Sikwese amegiza Watendaji wote wa vijiji ambao hawajahudhulia kikao cha leo waandike barua za maelezo na nakala iende kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Vilevile hakusita kukemea tabia ya Watendaji pamoja na Maafisa wengine kuvaa mavazi yasiyo rasmi wawapo maofsini. Amesema iwe marufuku uvaaji wa mavazi aina ya Dera au nguo za kubana ( jinsi za kubana), viatu vya wazi (open shoes au sandal) pamoja mabuti (Rain boots), huku akisisitiza sana kuacha kufanya kazi kwa mazoea.


No comments:

Post a Comment