Tuesday, March 26, 2024

BODI YA NYAMA YAONYA WAUZAJI WA NYAMA WANAOPULIZA DAWA YENYE SUMU KWENYE MABUCHA

Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Nyanda za Juu Kusini imepiga marufuku wauzaji wa bucha za nyama kuachana na tabia ya kupuliza dawa zenye sumu ili kulinda afya za walaji.

Ofisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Mpoki Alinanuswe amesema jana mkoani hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kitendo cha wauzaji kupuliza sumu kunaweza kuleta madhara makubwa kwa walaji huku akibainisha watu 10 wamechukuliwa hatua katika Mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Tulifanya ukaguzi maalum katika maeneo ya machinjio, mabucha,magari, na pikipiki zinazotumia kusafirisha nyama katika maeneo mbalimbali katika Mikoa hiyo na kubaini changamoto mbalimbali na tayari tumetoa maelekezo” amesema.

Wakati huo amewataka wauzaji wa nyama kutekeleza agizo la kuwataka kutumia vifaa vya kisasa kucharanga nyama na kuachana na tabia ya kutumia magogo ambayo sio salama kwa afya za walaji.

“Tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara lengo ni kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama sambamba na wafanyabiashara bucha kuzingatia kanuni za afya".

Amesema katika zoezi la ukaguzi walilifanya katika maeneo ya machinjio wamebaini kutokuwepo kwa mazingira yasiyo rafiki kwa baadhi ya machinjio kutokana na usimamizi usio mzuri wa Halmashauri.

Muuza bucha ya nyama eneo la Soweto Jijini hapa Athanas Nassoro ameomba elimu itokewa na sio kwamba wanafanya kwa bahati mbaya lengo ni kuondoa wingi wa nzi wanaozaliana.

No comments:

Post a Comment