Friday, March 22, 2024

MBEYA - UWSA YACHANGIA MABATI UJENZI SEKONDARI NA OFISI SERIKALI YA MTAA


Katika kilele cha kuadhimisha wiki ya Maji duniani Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYA - UWSA) imegusa jamii kwa kutoa msaada mabati bando nane kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

Msaada huo umetolewa kwa makundi mawili ikiwepo ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa Tonya Kata ya Ilomba na Kata ya Utengule Usongwe kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ihombe iliyopo jirani na chanzo cha Maji Ilunga.

Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Maji, Mhandisi Barnabas Konga amekabidhi msaada huo jana Machi 22 , mwaka huu katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Mamlaka hiyo.



Konga amesema huo ni utaratibu wa Mamlaka hiyo kila mwaka ifikapo Machi 16 mpaka 22 wamekuwa na utaratibu wa kuchangia shughuli za maendeleo ikiwa ni kuadhimisha wiki ya Maji Duniani.

"Huu ni utaratibu wetu kwa kila mwaka tunaendelea kuigusa jamii na kuchangia miradi ya maendeleo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kama kurejesha sehemu ya faida kwa wateja wetu” amesema.

Kwa upande wake Diwani Kata ya Ilomba Jijini  Tonebu Chaula amesema msaada huo utasaidia kupaua ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Tonya Jijini hapa ambayo umejengwa kwa nguvu za Wananchi.

“Nishukuru sana Mamlaka ya Maji kwani nilileta maombi ya msaada wa mabati baada ya Wananchi kutumia nguvu kazi na michango mbalimbali kujenga Ofisi ambayo imefikiwa  hatua ya kupaua ambapo leo nimekabidhiwa naa niaba ya Wananchi” amesema huku akihaidi kuendelea kutoa ushirikiano.

Naye Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, Yona Japhet ameshukuru Mamlaka kwa  kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari kwani itakuwa chachu katika kuchochea sekta ya elimu na vijana kufanya vizuri katika masomo.

Amesema Shule hiyo imejengwa eneo ambalo kipo chanzo cha Maji Ilungu watahakikisha wanaendelea kukilinda dhidi ya watu wataofanya shughuli za kijamii.

No comments:

Post a Comment