Umeme wageuza vijiji kuwa vituo vya maendeleo; shule, biashara na kilimo vyanufaika…
Na Sanula Athanas aliyekuwa Shinyanga
KIJIJI cha Masunula katika Kata ya Usule, Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, kina historia inayofanana na mamia ya vijiji vingine nchini.
Kilianzishwa mwaka 1974 kupitia Operesheni Vijiji (1973-1976), mkakati wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, uliolenga kuwakusanya wananchi katika maeneo maalum ili kurahisisha utoaji huduma za msingi kama elimu, afya, maji na miundombinu mingine ya maendeleo.
Kwa miongo mitano, wakazi wa Masunula waliishi maisha ya kawaida ya vijijini yaliyotawaliwa na matumizi ya mafuta ya taa kwa mwanga, mashine zinazotumia dizeli kwa shughuli za uzalishaji na uhaba wa huduma nyingi za kisasa zilizokuwa zikionekana kama haki ya wakazi wa mijini pekee.
Lakini mwishoni mwa mwaka 2020,
historia ya kijiji hicho kilichoko umbali wa Km 33.5 Kusini Magharibi mwa Mji
wa Shinyanga ilianza kuandikwa upya.
Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umeme ulifika Masunula. Tangu wakati huo, maisha ya wananchi yamebadilika kwa kasi kubwa kiasi kwamba baadhi yao wanaamini tofauti iliyobaki kati ya kijiji na mji ni jina tu.
Katika Kitongoji cha Bukengwa, kijijini Masunula, Nyanzobe Ng’wandu anakumbuka kwa huzuni lakini pia kwa tabasamu maisha ya kabla ya ujio wa umeme vijijini.
Anasema miaka michache iliyopita usalama wa mifugo yao ulikuwa ukitegemea moto mkubwa uliowashwa usiku kucha karibu na mazizi ili kuwafukuza fisi waliokuwa wakivizia mifugo.
“Umeme umetuondolea adha nyingi. Kabla ya umeme kuletwa hapa kijijini, ilikuwa ni lazima kila siku hapa nyumbani tukoke moto mkubwa usiku karibu na zizi kwa kutumia magogo makubwa ili fisi wasije kunyemelea mifugo,” anasema.
Leo hali imebadilika kabisa. Nyanzobe anayejitambulisha ana umri wa miaka 61, mama wa watoto watatu na bibi wa wajukuu 16, anasema:
“Kwa sasa hatuna utaratibu huo tena. Umeme unamulika kila kitu. Fisi hawaji tena kunyemelea mifugo yetu maana kuna mwanga.”
Kiusalama na kimazingira, hii ina maana kwamba hofu ya kushambuliwa na fisi usiku haipo tena, magogo hayatumiki tena na misitu imesalimika.
Nyanzobe anaeleza kuwa mbali na usalama wa mifugo, umeme umeondoa changamoto kubwa ya mawasiliano iliyokuwa ikiwakabili wakazi.
“Kitongoji chote hiki kilikuwa na kaya moja tu iliyokuwa na umeme wa jua. Hapo ndipo watu wote wa kitongoji hiki tulipatumia kupanga foleni ya kuchaji simu kwa malipo ya Sh. 200 kwa kila simu,” anasimulia.
Anasema hata burudani ilikuwa bidhaa adimu kwa wakazi wa Kitongoji cha Bukengwa.
“Kwenye ile kaya iliyokuwa na umeme wa jua, ndipo mahali pekee kwa kitongoji hiki wapenda mpira walikuwa wanakwenda kuangalia mechi kwa malipo ya Sh. 500 kwa mechi,” anasema.
Lakini sasa hali imebadilika. Nyanzobe anasema: “Leo kaya nyingi katika kitongoji hiki zina umeme. Na walio na TV (televisheni) ni wengi.”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bukengwa, Kajala Kajigo, maendeleo ya upatikanaji umeme katika eneo hilo yanaonekana dhahiri.
Anasema kitongoji hicho kina jumla ya kaya 48, ambapo kaya 35 tayari zimeunganishiwa umeme, sawa na asilimia 72.9 ya kaya zote.
Hata hivyo, bado kuna kaya 13 zinazotamani kunufaika na huduma hiyo muhimu. Miongoni mwao ni kaya hizo ni ya Sinzika Mala, ambaye anasema kikwazo kikubwa si kukosekana kwa umeme katika kitongoji chao, bali umbali wa makazi yao kutoka kwenye barabara zilikopitishwa nguzo za umeme.
“Tunatamani kuunganishiwa umeme kama wenzetu, lakini nyumba zetu zipo mbali na njia ya nguzo. Tunaamini siku moja huduma hii itatufikia pia,” Mala anasema.
TIJA KIUCHUMI
Eneo lingine lenye mageuzi yanayoonekana kwa haraka zaidi ni uchumi wa wananchi. Mmoja wa wamiliki wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka katika Kijiji cha Masunula, Jibushi Ng’henhagula, anasema aliona fursa mara tu baada ya umeme kufika kijijini.
“Kabla ya umeme kulikuwa na mashine moja tu hapa kijijini iliyokuwa inatumia dizeli. Kwa hiyo umeme ulipofika tu Masunula Novemba 2020, Februari 2021 nikafungua mashine yangu hii,” anasema.
Anaeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta nchini kunakoshuhudiwa hivi sasa kungekuwa na madhara makubwa zaidi kwa wananchi wa vijijini kama wasingekuwa na mashine za umeme.
“Kwa sasa bei ya mafuta haishikiki sokoni. Fikiria kama kusingekuwa na mashine hizi za umeme za kukoboa na kusaga nafaka huku kijijini hali ingekuwaje katika kipindi hiki. Umeme umetusaidia sana,” anasema.
Matunda ya uwekezaji huo yameonekana katika maisha yake ndani ya kipindi cha miaka sita tangu umeme ufike kijijini kwao.
Kupitia mashine yake ya kusaga na kukoboa nafaka, Jibushi anasema amekuwa akipata pumba kwa wingi ambazo huzitumia katika shughuli nyingine ya ufugaji wa kibiashara.
Anasema hununua ng’ombe katika minada mbalimbali mkoani Shinyanga, kisha huwanenepesha kwa kutumia pumba zinazotokana na shughuli zake za ukoboaji nafaka kabla ya kuwasafirisha kwenda katika mnada mkubwa wa Pugu jijini Dar es Salaam ambako hupata soko na bei nzuri zaidi.
Kutokana na mafanikio hayo, Jibushi amebadilisha maisha ya familia yake. Amejenga nyumba ya kisasa kijijini Masunula kwa ajili ya makazi, huku pia akijenga nyumba nyingine ya biashara katika Mji Mdogo wa Kagongwa wilayani Kahama.
Kwa mtazamo wake, umeme vijijini haujaleta mwanga pekee, bali umefungua milango ya fursa za kiuchumi zilizowawezesha wananchi wengi kuongeza kipato, kuwekeza na kuboresha maisha yao.
MTENDAJI WA KIJIJI
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Masunula, Rachel Mwakibete, anasema ujio wa umeme umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
“Wanakijiji wamefurahia huduma hii, wamepunguza gharama za kutumia mafuta ya taa ambayo mbali na kuwa ni nishati chafu inayoathiri afya, ni hatari kwa usalama wa nyumba zao.
“Kwa sasa wana uhakika wa mwanga wa umeme nyakati za usiku. Tuna mashine nne sasa hapa kijijini za kukoboa na kusaga nafaka, zote zinatumia umeme. Kupitia mashine hizi ajira zimezalishwa,” anasema.
Anataja pia kuongezeka kwa saluni za kisasa kutoka moja hadi nane, huku biashara nyingine nyingi zikianza kuchipuka kutokana na uhakika wa umeme.
“Tuna saluni nane sasa hapa kijijini, awali tulikuwa nayo moja ambayo ilitegemea umeme wa jua. Siku kukiwa na mawingu kuanzia asubuhi hadi jioni, maana yake siku hiyo hakuna huduma,” anasema.
UMEME SHULENI
Faida za umeme hazijaishia katika biashara na maisha ya nyumbani pekee. Sekta ya elimu nayo imeendelea kuvuna matunda.
Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na kuwapo umeme katika Shule ya Msingi Masunula ni Japhet Ndekeja, ambaye alihitimu darasa la saba mwaka jana.
Japhet anasema programu za masomo ya usiku zilizowezeshwa na umeme zilikuwa na mchango mkubwa katika ufaulu wao.
“Umeme ulitusaidia kuwa na programu za masomo ya usiku shuleni. Tulikuwa tunasoma hadi saa nne usiku,” anasema.
Matokeo ya mkakati huo ni makubwa. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masunula, Daud Bukela anasema wanafunzi wote 30 (wasichana 12) walifaulu kwa Daraja “A”.
Katika kundi hilo, wanafunzi 18 walichaguliwa kujiunga na shule za bweni Januari mwaka huu, huku Japhet aking’ara kihistoria.
Mwalimu Mkuu Bukela anasema Japhet amekuwa mwanafunzi wa pili kutoka Shule ya Msingi Masunula kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe mkoani Morogoro.
Simon Nkuli ndiye mwanafunzi wa kwanza kutoka Masunula kuchaguliwa kujiunga na Mzumbe, moja ya shule za vipaji maalumu zenye ushindani mkubwa nchini. Sasa yuko kidato cha tatu, mafanikio yake kielimu yakiwa sehemu ya matokeo ya ujio wa umeme vijijini.
Mwalimu Mkuu Bukela anasema kabla ya ujio wa umeme, walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kuchapisha mitihani. Leo wanafanya kazi hiyo shuleni.
Anasema walimu sasa wanatumia kompyuta, projekta na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji.
Vilevile, kama ilivyoelezwa awali na mhitimu wa shule hiyo Japhet, Mwalimu Mkuu Bukela anasema wanafunzi wa madarasa ya mitihani hupata muda wa ziada wa kujifunza hadi saa nne usiku kupitia kambi maalum za masomo.
Hali kama hiyo imeonekana pia katika Shule ya Msingi Nzagaluba iliyoko Kata ya Usanda wilayani Shinyanga. Mwalimu wa Taaluma, Maduhu John, anasema umeme umebadili mbinu za kufundisha TEHAMA.
“Tayari madarasa yameunganishwa umeme. Mwalimu anaweza kutumia laptop (kompyuta mpakato) yake na vifaa vingine kufundisha wanafunzi TEHAMA kwa vitendo tofauti na awali ambapo kabla ya kupata umeme miaka mitano iliyopita, tulizoea kufundisha watoto kwa nadharia tu,” anasema.
HUDUMA YA MAJI
Mbali na elimu, umeme umeimarisha upatikanaji maji. Kijiji cha Masunula ni mfano hai wa mabadiliko hayo.
Ofisa Mtendaji Rachel anasema kisima kirefu cha kijiji kinatumia mota za umeme kusukuma maji kwenda tangi kuu kabla ya kusambazwa kwa wananchi.
“Matokeo yake ni kupungua kwa muda wa kusubiri maji, kupungua kwa gharama za uendeshaji na kuongezeka kwa upatikanaji huduma hii muhimu,” Rachel anasema.
Hii inaendana pia na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG) ya mwaka 2015, hususan Lengo la Saba (SDG 7) linalotaka kuhakikisha upatikanaji nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.
FURSA UJASIRIAMALI
Kijijini Nzagaluba, umeme umefungua milango mipya ya kujiajiri na kujiongezea kipato kwa wananchi.
Miongoni mwa walionufaika ni Jumanne Njile (50), fundi seremala ambaye aliona fursa mpya mara tu baada ya kijiji hicho kuunganishiwa umeme mwaka 2018.
Akiwa ndani ya karakana yake yenye sauti za mashine na harufu ya vyuma vinavyokatwa, Njile anasimulia namna maisha yake yalivyobadilika baada ya ujio wa umeme.
“Mimi tangu zamani ni seremala. Umeme ulipokuja nikaachana na mbao, nikaamua kutumia vyuma,” anasema.
Njile kwa sasa hutengeneza mikokoteni, mashine za kupukuchua mahindi pamoja na kazi nyingine za uchomeleaji vyuma ambazo zimekuwa na soko kubwa kijijini na maeneo jirani.
Kwa mujibu wa Njile, biashara hiyo imekuwa chanzo kikuu cha kipato cha familia yake.
“Kipato changu, inategemeana na mwezi, kwa wastani unaweza kupata Sh. 500,000 hadi 600,000 kwa mwezi,” anasema.
Njile anasema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni mtaji wa kupanua biashara yake.
“Mtaji ni tatizo. Nikipata mtaji mkubwa, nitanunua mashine ya kukoboa mpunga. Mashine ya kusaga nafaka ninayo. Ninahitaji mashine kubwa ya kukoboa. Gharama yake ni Sh. milioni 12,” anasema.
Licha ya changamoto hiyo, mafanikio yake yanaonekana. Njile ni baba wa watoto 10 kutoka katika familia yenye wake wawili. Kupitia kipato kinachotokana na shughuli zake za ujasiriamali, amefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa, kibanda cha kuonesha mechi za soka na duka la rejareja.
Anasema wananchi wengi wa Nzagaluba kwa sasa wanatumia umeme kwa matumizi ya nyumbani, huku wengine wakianza kuutumia kama nyenzo ya kuzalisha kipato.
Miongoni mwao ni Emmanuel Ngasa, mhitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mpanda mwaka 2023 na baba wa mtoto mmoja wa kike.
Akiwa na mtaji wa Sh. 600,000 pekee, miaka miwili iliyopita, alianza shughuli za uchomeleaji vyuma baada ya kununua mashine mbili za msingi; moja ya kukatia vyuma na nyingine ya kuchomelea.
Leo hii Ngasa (25) hutengeneza milango, mageti, madirisha na vitanda vya chuma kwa wateja kutoka Nzagaluba na maeneo jirani, shughuli inayomwezesha kujipatia kipato na kuhudumia familia yake.
“Kwa sasa bado najijenga. Nikipata mtaji mkubwa zaidi natamani kuwa na karakana kubwa ya kisasa pamoja na duka la vifaa vya ufundi. Hivi sasa nikipata oda, mara nyingi nalazimika kwenda kununua vifaa sehemu nyingine,” anasema.
Moja ya mashine za kusaga na kukoboa zilizoko kijijini Masunula. PICHA: SANULA ATHANAS
VINYWAJI BARIDI
Kijijini Mishepo, Kata ya Mwantini wilayani Shinyanga, umeme uliofikishwa na REA mwaka 2025 umeanza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa mwanakijiji Godfrey Mbogo, huduma za kukoboa na kusaga nafaka zimekuwa nafuu zaidi kulinganishwa na enzi za mashine zinazotumia mafuta.
“Tulikuwa tunalipa hadi Sh. 1,600 kukoboa na kusaga debe moja la mahindi la kilo 20, lakini sasa tunalipa Sh. 1,000 tu. Hii tofauti ya Sh. 600 inaweza kuonekana ndogo kwa watu wa mjini, lakini kwetu ina maana kubwa,” anasema.
Anaeleza kuwa mashine za kisasa zinazotumia umeme zimeongeza ubora wa huduma kwa kutoa “mchele ulionyooka, usiovunjika na usiokuwa na mchanga”.
Vilevile, anasema ujio wa umeme umefungua milango ya fursa mpya za kiuchumi, zikiwamo biashara za kuchaji simu za wananchi ambao vitongoji vyao havijafikiwa na umeme, saluni na uuzaji vinywaji baridi, hatua inayochochea maendeleo na kuifanya Mishepo kufanana zaidi na mazingira ya mjini.
KATIBA YA NCHI
Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haitaji umeme moja kwa moja kama haki ya msingi, Ibara ya 9(1)(a) na (i) inaelekeza serikali ihakikishe rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote na shughuli za kiuchumi ziendeshwe kwa lengo la kuondoa umaskini, ujinga na maradhi.
Vilevile, Ibara ya 11(1) ya Katiba inaelekeza mamlaka za umma kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kupata huduma muhimu kwa ustawi wao.
Ofisa wa Haki za Binadamu na Biashara kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Clay Mwaifwani, anatoa tafsiri ya kitaaluma.
Anasema upatikanaji umeme ni sehemu muhimu ya utekelezaji masharti hayo ya kikatiba kwa kuwa unawezesha utoaji huduma za elimu, afya, maji na shughuli za uzalishaji mali.
Kisheria, Sheria ya Nishati Vijijini Na. 8 ya mwaka 2005 ndiyo iliyoanzisha Mfuko wa Nishati Vijijini na baadaye kuunda Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mwaka 2007 kwa jukumu la kuharakisha upatikanaji umeme katika maeneo ya vijijini.
MIONGO MIWILI
Miaka 19 iliyopita, hali ya upatikanaji umeme vijijini ilikuwa ya kusikitisha. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi anarejea takwimu za wizara hiyo zinazoonesha kuwa wakati REA inaanza kazi mwaka 2007, kiwango cha upatikanaji umeme vijijini kilikuwa asilimia mbili pekee.
Leo hali imebadilika. Waziri Ndejembi anasema upatikanaji umeme nchini umefikia asilimia 85.5 kitaifa huku maeneo ya vijijini yakifikiwa kwa asilimia 78.1.
Waziri Ndejembi anaipongeza REA kwa kutimiza lengo la kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara, huku vitongoji 40,182 kati ya 64,359, sawa na asilimia 62.4, vikiwa vimefikiwa na huduma hiyo.
Anasema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, anasema kwa sasa wana miradi mikubwa 13 inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku kukiwa na kandarasi 150 zinazolenga kupeleka umeme katika vitongoji 17,000.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeitambua nishati kama moja ya nguzo kuu za maendeleo ya taifa.
Dira hiyo inalenga kuwa na mfumo wa nishati safi, wa kuaminika, wa gharama nafuu na unaoweza kuhimili changamoto za siku zijazo.
Mabadiliko yanayoshuhudiwa leo katika vijiji vya Masunula, Mishepo, Nzagaluba na maeneo mengine mengi nchini yanaibua kumbukumbu za mwaka 1979. Nguli wa fasihi ya Kiswahili, Profesa Euphrase Kezilahabi, aliandika na kuchapisha riwaya yake maarufu Gamba la Nyoka.
Kupitia riwaya hiyo iliyoangazia harakati za ujamaa vijijini, Profesa Kezilahabi alionesha kwa kina changamoto za maendeleo vijijini na kusisitiza umuhimu wa serikali kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, zikiwamo nishati, elimu, maji na afya.
Kupitia wahusika wake vijana waliokuwa wahitimu wa vyuo vikuu, Profesa Kezilahabi alionesha namna ambavyo ukosefu wa huduma za msingi ulivyowafanya wengi kutotamani kuishi na kufanya kazi katika vijiji vya ujamaa vilivyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.
Takribani nusu karne baadaye, ujio wa umeme vijijini umeanza kubadilisha simulizi hiyo.
Mashine za kisasa za kusaga na kukoboa nafaka, saluni, vituo vya kuchaji simu, biashara za vinywaji baridi na shughuli nyingine za kiuchumi zinazochipuka vijijini zinaashiria kupungua kwa tofauti iliyokuwapo kwa muda mrefu kati ya maisha ya mijini na vijijini.
Hivyo, maendeleo yanayotokana na upatikanaji umeme vijijini yanaonekana kutafsiri katika vitendo maono ambayo Profesa Kezilahabi aliyabeba ndani ya Gamba la Nyoka - kwamba kijiji kigeuke kuwa kitovu cha fursa, badala ya kuwa eneo la wananchi kusukumwa kuhama na kukimbilia mijini kutafuta huduma na maisha bora.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi. Picha na Wizara ya Nishati



No comments:
Post a Comment