Monday, August 12, 2024

WANANCHI RUIWA NA MAHONGOLE WAOMBA KUTENGENEZEWA DARAJA LILILOHARIBIWA NA MAFURIKO

Wananchi wa Kata za Ruiwa na Mahongole Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wameiomba Serikali kuwajengea daraja jingine eneo la Msikitini linalounganisha Kata ya Ilongo, Ruiwa na Mahongole lililoharibiwa na mvua za elinino mapema mwaka huu.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema daraja hilo kwa sasa ni hatarishi kwa waendesha bodaboda ambao wametengeneza kiunganishi cha muda kwa kutumia mbao na kwa sasa halina uwezo wa kupitisha magari hivyo kufanya gharama kubwa za nauli.

Diwani wa Kata ya Ruiwa Kassim Mtale amesema kukatika kwa daraja hilo kumeongeza umbali wa kilometa tatu kutoka daraja hilo kufika Ilongo.

Mtale amesema taarifa imetolewa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali pamoja na Wakala wa barabara Vijijini (TARURA) ambao walifika kwa ajili ya kufanya tathimini.

Aidha amesema kama daraja halitajengwa msimu huu wa kiangazi hali itakuwa tete kipindi cha masika hasa kwa wanafunzi wanaotoka Ilongo kwenda kusoma Kata za Ruiwa na Mahongole.

Mhandisi Anyitike Kasongo ni Meneja wa wakala wa barabara Vijijini (TARURA) Wilaya ya Mbarali amekiri kukatika kwa daraja hilo na kwamba tathimini imefanyika kinachosubiriwa kwa sasa ni fedha ili kurejesha mawasiliano ya wananchi wa Ruiwa na Mahongole.

Daraja hilo ni kiungo muhimu katika usafirishaji wa mazao na pembejeo kwenda na kutoka Kata hizo tatu.

No comments:

Post a Comment