Katika kulelea siku ya Wanawake duniani ambayo kilele ni Machi 8 mwaka huu Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF _Net) Mkoa wa Mbeya umetoa misaada mbali mbali kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima cha Nuru na St. Allamano .
Msaada huo umekabidhiwa jana Machi 4,2024 huku wakiomba Serikali kulegeza masharti ya mabadiliko ya sheria za bima afya kwa vituo vya kulelea watoto yatima.
Mwenyekiti wa Mtandao huo SP. Kanen Muro amesema kuwa sheria hiyo inavitaka vituo hivyo kuwa na watoto wasio chini ya 100 ndipo wakatiwe bima ya Sh 59,400.
“Tuombe Serikali ilione hilo ili watoto waweze kupata huduma bora za afya kwani kwenye kituo cha Nuru kina mahitaji makubwa sana na hakijafikia watoto 100 waliopo ni 33 wakiwepo walemavu” amesema.
Aidha amesema kuwa lengo la kutembelea vituo hivyo na kutoa mahitaji ni kuwatia Moyo watoto wenye changamoto na wasimamizi wa vituo ikiwa ni wiki kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambayo kilele ni Machi 8 mwaka huu.
Naye Msaidizi wa Dawati la Jinsia na watoto, Inspekta Loveness Mtemi ameitaka jamii kuwa na hofu ya Mungu ya kuachana na tabia ya kutupa watoto ambapo kwa kituo cha Nuru pekee takwimu zinaonyesha asilimia 80 ya watoto wanafikishwa wametupwa na kutelekezwa.
“Wanaume na Wanawake kuweni na hofu ya Mungu mnazaa na kufikia hatua ya kutupa watoto kwa kweli inasikitisha sana niombe jamii ijitokeze kusaidia vituo vinavyotoa huduma kwa watoto yatima” amesema.
Meneja wa kituo cha Nuru ,Mary Kassim amesema kuwa asilimia 80 ya watoto wanaopokelewa ni kuanzia siku 0 mpaka miaka 5 ambao wametupwa na wazazi wao kufuatia changamoto mbalimbali.
Amesema licha ya kutunza watoto yatima changamoto kubwa ni bima ya afya kufuatia mabadiliko ya sheria iliyofanyiwa marekebisho ikiwepo gharama za vifurushi..
“Hii ni changamoto kubwa kwani kwa vituo tunapaswa kuwa na watoto yatima 100 sisi kituo chetu kina watoto 33 jambo ambayo linatupa wakati mgumu panapo hitajika huduma inapojitokeza mtoto kuugua ghafla” amesema.
Mary ameomba Serikali kuangalia upya kwenye vituo vya kulea yatima kwa kulegeza masharti ili kuwezesha kundi la watoto wenye uhitaji kupata huduma.
Mtoto yatima Joel Joel ameomba Serikali na wadau mbalimbali nchini kulitazama kundi hilo ambalo limekosa mapenzi kwa wazazi kwa kujitoa kuwasaidia mahitaji mbalimbali kupitia vituo vinavyowahudumia.
No comments:
Post a Comment