Tuesday, March 19, 2024

MBEYA KUONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAJI MACHI 2025

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (MBEYA - UWSA) imesema mradi mkubwa wa kimkakati wa chanzo cha mto Kiwira Wilayani ya Rungwe utakamilika ifikapo mwezi Machi 2025.

Mradi huo utakaogharimu Sh 250 bilioni mpaka kukamilika ambapo katika awamu ya kwanza zitatumika Sh 119 bilioni katika hatua mbalimbali ikiwepo usanifu na ujenzi huku ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 117.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mhandisi Barnabas Konga amesema, Jana mara baada ya kutembelea eneo la utekelezaji wa mradi huo wilayani Rungwe, ikiwa ni sehemu ya kuelekea wiki ya Maji Duniani ambayo iliyoanza Machi 16 mpaka 22 mwaka huu.

“Hii ni wiki ya Maji pia tunazungumzia miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa na mafanikio makubwa ikiwepo kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa chanzo cha mto Kiwira” amesema.

Mhandisi Konga amesema mahitaji ya Maji kwa Mkoa wa Mbeya na Mji wa Mbalizi ni lita milioni 99 huku uwezo wa kuzalisha ni lita milioni 66.4 kutoka kwenye vyanzo 20 vilivyopo.
“Tunataraji ifikapo mwezi Machi 2025 tatizo la maji itakuwa hadithi kwa wananchi hali ambayo itachochea shughuli za kiuchumi kwa jamii” amesema.

Mhandisi mshauri mkaziwa mradi wa Kiwira, Audax Rweyamamu amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 10 na umejengwa kwa mfumo wa kubuni ambapo ndio utaratibu wa sasa nchini.
Amesema pia utekelezaji wa kuchimba matenki mawili ya kuhifadhia Maji unaendeleaje katika kata ya New Forest na Sistila yenye uwezo wa kutunza maji lita 5,000 kwa kila moja.

Naye ofisa uhusiano na Mahusiano, Neema Stanton amesema mradi huo utakuwa mwarobaini wa hadha ya Maji katika maeneo mbali kwani ni mradi wa kimkakati.

No comments:

Post a Comment