Sunday, March 3, 2024

HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA KUTOA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA MASIKIO, PUA NA KOO

Wasimamizi hospatali za Rufaa za Mikoa nchini wameagizwa kuhakikisha uwepo wa vifaa ambavyo vitatumika kutoa matibabu ya masikio, koo na pua ili kufanikisha utolewaji wa huduma bora kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo Machi 03, 2024 na Mgeni rasmi Dkt. Maisara Karume wakati akihutubia kwaniaba ya Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya siku ya usikivu duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mbeya katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

"Ili kufanikisha utolewaji endelevu wa huduma hizi kwa wananchi wote, nawaagiza wasimamizi wa hospitali zote za rufaa kuhakikisha uwepo wa vifaa ambavyo vitatumika kutoa matibabu ya masikio, koo na pua. Vivyo hivyo Waganga Wakuu na Halmashauri kusimamia vituo vyote vya huduma za afya ya msingi vilivyo katika maeneo yao kwa kuweka bajeti za vituo vyao fedha na kununua vifaa kwaajili ya kuwezesha kufanya uchunguzi wa sikio la nje, mfereji wa sikio na ngoma ya sikio" amesema Dkt. Karume.

Pia ameongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau watahakikisha watumishi wa afya wanapewa mafunzo maalum ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya usikivu, kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha huduma za kuzuia na kuthibiti magonjwa yanayosababisha kupotea kwa usikivu kwa watu wazima na watoto.

Sambamba na hilo Dkt. Karume ameongeza kuwa Hospitali zote za Rufaa za Mikoa zinatoa huduma za kibingwa za masikio na kuahidi kuwa watumishi wa afya watajengewa uwezo ili waweze kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi wa masikio na usikivu.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Amina Mfaki amesema ofisi yake itaendelea kuienzi siku hii kwa kuendelea kuboresha mifumo ya utambuzi wa watoto wenye ulemavu, kupitia watoa huduma wa ngazi ya jamii na watendaji wa kata pamoja na vijiji au mitaa kwa kuwatambua na kuanza matibabu mara moja pindi wanapobainika kuwa na changamoto ya aina yeyote.

Akitoa salamu katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt. Godlove Mbwaji ameshauri wataalamu kutoa elimu kwenye maeneo mbalimbali ili kuzuia changamoto ya kupoteza usikivu pi kubuni kifaa maalumu cha kuwatambua watu wenye changamoto ya usikivu.

 
"Wataalamu waendelee kuweka mikakati ya uzuia hii changamoto kwa kutoa elimu hasa maeneo yenye kiwango cha juu cha sauti ili kuzuia changamoto ya usikivu, pia kwa upande wa sheria na kanuni ziwepo na kutusaidia kwani ni vizuri kutibu na pia kuzuia. Lakini pia kuwepo na alama yeyote maalumu ya kuwatambua wenzetu wenye changamoto ya usikivu kama ilivyo kwa walemavu wa macho" amesema Dkt. Mbwanji.

Awali akisoma risala wakatia wa maadhimisho hayo, Katibu wa Jumuiya ya Wataalamu wa masikio, pua na koo Tanzania Dkt. Raphael Gabriel ameshauri hospitali zote za mikoa kuwa na madaktari bingwa wa masikio, pua na koo, mtaalamu wa kupima usikivu na kufundisha lugha na tiba pamoja na mashine za kupimia usikivu.

Maadhimisho ya siku ya usikuvu duniani huadhimishwa Machi 03 kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa masikio na usikivu sambamba na kutoa elimu ya kuzuia upotevu wa usikivu. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni "Tubadili mtazamo: Tufanye huduma thabiti za masikio na usikivu kwa wote".




No comments:

Post a Comment