Thursday, October 24, 2024

CHAUMA YAWAITA VIJANA NA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI


Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) Mkoa wa Mbeya Ipyana Njiku, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi bora wa serikali za mitaa katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Njiku ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji utakaofanyika Novemba 27, 2024.

"Tumeona muamko mdogo wa watu kujitokeza kupiga kura lakini niwambie hii ni haki yetu ili kupata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu", amesema Ipyana Njiku.

Pia Njiku amewataka wananchi kuwa chachu ya kutunza amani ya nchi wakati na baada ya chaguzi ili kuendelea kuwa Taifa moja na kuwaalika wenye nia na uwezo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.

"Haki ya kupiga kura ni silaha muhimu kwa kila raia katika kuhakikisha uongozi bora maendeleo yetu, bila kura unatoa nafasi kwa wengine kuamua nani awe kiongozi wao kwahiyo tunaomba siku ya uchaguzi tujitokeze kwa wingi kwenda kuchagua viongozi bora. Pamoja na kupiga kura lakini hii ni fursa kwa watu wenye sifa, dhamira safi, uadilifu na utayari kuwatumikia wananchi kwa kujitokeza kugombea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA", amesema Njiku.

No comments:

Post a Comment