Monday, October 21, 2024

BITEKO MGENI RASMI WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA KITAIFA MBEYA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini Dotto Biteko anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa ambayo yatafanyika Mkoa wa Mbeya na kuhusisha Taasisi mbalimbali za kifedha.

Maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi kuanzia Oktoba 22 mpaka 26 mwaka huu katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20, 2024 Kamishna msaidizi wa Idara ya Uendeshaji sekta ya fedha kutoka wizarani Janeth Hiza amesema lengo ni kutekeleza mpango mkuu wa maendeleo ya sekta hiyo kwa mwaka 2020/21 na 2029/30.

Alisema kupitia programu hiyo Wizara imeweka mikakati ya kutoa elimu ya fedha za umma kwa kushirikiana na wadau wa taasisi za kibenki ikiwa ni mpango mkakati wa miaka mitano.

"Lengo ni kuwafikia watanzania wote kupata elimu ili kuwa na uelewa mpana na mikakati ya serikali ni  kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanakuwa na uelewa wa pamoja" alisema.

Janeth amesema asilimia kubwa ya watanzania walio wengi hawatumii huduma za fedha kufuatia tafiti iliyofanywa na Taasisi ya FinScope kubainia asilimia 53.5 pekee kutumia huduma hizo.

Ofisa uhusiano wa elimu kwa umma kutoka Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA) Stella Anastazia ametaka wananchi watumie fursa ya maadhimisho ya maonyesho hayo kupata elimu.

Meneja Idara ya fedha na uendeshaji Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Maristella Kamuzora amesema elimu mbalimbali itatolewa kwa wananchi kujua masuala mbalimbali ya kifedha.

Abdul Njahidi  ambaye ni Ofisa uhusiano wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSF) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu amehamasisha wananchi kujitokeza kupata elimu kupitia maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment