Monday, October 7, 2024

PROF. KABUDI AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI WA BILIONI 4.8 MBEYA

Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Ilungu Kata ya Utengule Usongwe Wilaya ya Mbeya.

Mradi huo una thamani ya zaidi ya Sh 4.8 bilioni na kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya-UWSA) ambao unatarajia kunufaisha wananchi 110,000 kutoka vijiji vitatu na kata nne.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ihango kata ya Utengule Usongwe Prof. Kabudi ameeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wanaondokana na changamoto ya maji.

"Nipongeze sana Mamlaka ya Maji Mbeya kwa kutekeleza mradi huu mkubwa ambao unakwenda kuwa mwarobaini kwa wananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa wakati" amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi pia ameagiza Mamlaka hiyo kuweka uzio eneo la mradi wa Ilungu na kufunga taa za sora ili kuimalisha ulinzi na usalama.

Wakati huo huo ametoa mwezi mmoja kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuboresha miundombinu ya barabara inayoelekea kwenye mradi wa Ilungu kutokana na umuhimu wake kwa jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji ya Maji  Mbeya Mhandisi, Gilbert Kayange amesema fedha za kutekeleza mradi huo zimetolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maji.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa upatikanaji wa huduma kutoka asilimia 88 mpaka 90.

Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza ameomba kuboreshwa miundombinu ya barabara ili kuchochea shughuli za kiuchumi kufuatia wananchi wanajihusisha na shughuli za kilimo cha kahawa jimboni kwake.

Mkazi wa Utengule Usongwe Joel Samweli amesema kitendo cha kufikishiwa huduma ya maji kutaleta chachu kwa wakinamama kutotumia muda mwingi kusaka maji na badala yeke kugeukia shughuli za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment