Tuesday, October 8, 2024

UJENZI MRADI WA MAJI MTO KIWIRA WAFIKIA ASILIMIA 35

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya umefikia asilimia 35 ambao unatarajia kunufaisha watu zaidi milioni 1.4.

Mkurugenzi uzalishaji na usambazaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya (MBEYA - UWSA) Mhandisi Barnabas Konga amesema jana wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kapudi.

Mradi huo utajengwa kwa miaka miwili ambapo ukikamilika utazalisha lita milioni 184 kwa siku na wananchi zaidi ya milioni 1.4 katika Mkoa wa Mbeya na Mji wa Mbalizi watanufaika kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

Mhandisi Konga amesema mradi huo utagharimu Sh bilioni 119 chini ya mkandarasi mshauri wa kampuni ya Ghw Consultant GmbH na kampuni ya ujenzi ya China Railway Construction Engineering Group.

Amesema kukamilika kwake kutaongeza tija ya upatikanaji wa huduma kutoka masaa 19 mpaka 23 kwa siku ikiwa ni kutekeleza lengo la 6 la maendeleo endelevu la umoja wa mataifa ifikapo 2030.

Akizungumza na maelfu mara baada ya kukagua mradi huo Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Kabudi amesema ameridhishwa na utekelezaji wake na kwamba utaleta tija kubwa kwa wananchi.

"Huu mradi wa pili wa Maji kutembelea katika ziara yangu nilianza Mbeya vijijini na sasa huu wa Kiwira eneo la tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 5 kutoka kwenye chanzo kikubwa nipongeze uongozi wa Mamlaka kwa kazi nzuri inayoonekana" amesema.

Prof. Kabudi pia ameonya jamii kuacha mara moja shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji na ukataji miti ovyo ili kuepukana na majanga ya ukame yanayoweza kusababisha upotevu wa rasilimali ya maji .

No comments:

Post a Comment