Thursday, October 3, 2024

MKUTANO WA MWAKA WA WAKUU WA MAMLAKA ZA KUPAMBANA NA RUSHWA KWA NCHI ZA SADC 2024 - LUSAKA, ZAMBIA

Wakati Dunia ikishuhudia majanga katika maeneo mbalimbali, Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC zimetahadharishwa kuwa makini kwani mikakati ya haraka inayoandaliwa kukabiliana na hali hiyo inaweza kutoa mianya ya rushwa.
 
Akizungumza Oktoba 2, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa mamlaka hizo jijini Lusaka - Zambia, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya SADC ya Kupambana na Rushwa (SADC Anti Corruption Committee - SACC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini - TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, amefafanua kuwa hatari ya uwepo wa vitendo vya rushwa inaweza kujitokeza wakati wa mchakato wa kupata na au kutoa misaada wakati wa dharura. 

“Hatua zote za mnyororo wa utoaji wa misaada ziko katika hatari ya rushwa kutokana na dharura inayokuwepo", alisema.


Wakuu wa Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC pamoja na Viongozi na wajumbe mbalimbali kutoka katika mamlaka hizo za Nchi 14 wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Katika Mkutano huo unaoongozwa na kaulimbiu: ‘ Strengtherning Anti Corruption in Disaster Risk Management and in Correctional Serviseces in the SADC Region ', Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alitaja aina za vitendo vya rushwa vinavyoweza kutokea katika mazingira hayo ya ‘udharura’ kuwa ni pamoja na udanganyifu, ubadhirifu wa misaada, kuingilia usajili wa walengwa, utendaji usio wa maadili katika ununuzi na kwamba pia hali hiyo inaweza kusababisha matumizi mabaya ya ngono - (Sextortion). 

Mkurugenzi Mkuu amesema, mlipuko wa magonjwa na mabadiliko ya tabia nchi unaongeza hali za dharura huku akisisitiza: “Hali hii inasababisha umuhimu wa kuwa na mikakati ya kudhibiti vitendo vya Rushwa katika ushughulikiaji na usimamizi wa dharura za majanga.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu amewashukuru nchi wanachama kwa ushirikiano na uungaji mkono wa juhudi za kikanda za Kuzuia na Kupambana na Rushwa na amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zambia, Monica Chipanta Mwansa (ambaye ni mwenyekiti aliyemaliza muda wake), kwa maendeleo yaliyopatikana wakati wa kipindi chake cha uongozi na hususan katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa SADC wa Kupambana na Rushwa (2023-2027), ambao unatekeleza malengo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa nchi za SADC.


Mkutano huu wa siku tatu umehudhuriwa na nchi wanachama 14 na umefunguliwa rasmi na Francis Chilinga, kutoka Wizara ya Sheria ya Zambia.

Tanzania inahudumu kama Mwenyekiti wa SACC kwa Mwaka 2024/ 2025 ikiwa ni mara ya pili baada ya kuhudumu kwa nafasi hiyo Mwaka  2017/2018 - mwaka ambao kamati hiyo ya SACC ilizinduliwa.

No comments:

Post a Comment