Tuesday, October 22, 2024

MEYA ISSA: JIEPUSHENI KUREJEA MIAKA 10 ILIYOPITA


Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa amewataka wananchi katika Jimbo la Mbeya mjini kutorejea miaka 10 iliyopita kwa kupiga kura kwa viongozi wasiofaa.

Issa amesema jana katika ziara ya Mbunge wa Mbeya Mjini Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwepo elimu na afya katika kata mbalimbali.

Amesema Taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na Mkuu 2025 hivyo wananchi wasifanye makosa badala yake wachague viongozi wa CCM akiwepo Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson na wenyeviti wa serikali za mitaa ambao wataleta tija katika maendeleo.

"Jamani msirudie  makosa ya miaka 10 iliyopita Jiji lilishikwa na upinzani na kupelekea kuchelewesha maendeleo lakini tunaona miaka mitatu ya Mama wa Connection tumepiga hatua kubwa" amesema.

Mkurugenzi Jiji la Mbeya John Nchimbi amesema serikali imetoa maelekezo Novemba 27, 2024 ni siku ya mapumziko kwa shule zote za msingi na sekondari ili kupisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa.

"Kufuatia mapumziko hayo vijana mlio na sifa ya kupiga kura mkashiriki lakini pia mkawe chachu ya kuwakumbusha wazazi kutumia haki ya kikatiba kushiriki zoezi hilo" amesema.

Awali Dkt. Tulia amehamasisha jamii kushiriki zoezi hilo muhimu ili kutekeleza haki ya kikatiba kuchagua kiongozi wanayemteka alete maendeleo ya kweli.

Amesema kiongozi mzuri anakuwa chachu ya kuleta na kunipunguzia kazi mimi kaka Mbunge katika kutekeleza miradi ya kimkakati.

Aidha Dkt. Tulia amesema kuwa ni wajibu wa watu walio na sifa za kugombea nafasi mbalimbali kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu ili kutimiza haki ya kikatiba.

No comments:

Post a Comment