Madaktari bingwa bobezi wa Mama Samia wanatarajia kuweka kambi ya siku tano ya kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Kambi hiyo imeratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Hosptali ya Rufaa kanda ya nyanda za juu kusini katika mikoa ya Songwe, Njombe, Songwe na Mbeya .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 2, 2025, Mganga mfawidhi wa Hosptali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya Dkt. Abdallah Mmbaga amesema kambi hiyo itaanza Mei 5 mpaka 9 mwaka huu.
Amesema madaktari bingwa bobezi wa Mama Samia wametoka katika Hosptali ya Taifa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Benjamin Mkapa na Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Dkt. Mmbaga amesema lengo ni kutoa huduma za kibingwa na kikobezi kwa wananchi wa mikoa ya nyanda za Juu Kusini hususani kwa wale wenye changamoto za kiafya zinazohitaji huduma za kitaalam.
Ametaja huduma zitakazotolewa ni pamoja na upasuaji wa kibingwa, magonjwa ya moyo, figo, saratani, macho, mifupa, masuala ya wanawake na uzazi, afya ya akili, huduma ya uchunguzi wa kina na elimu ya afya ya jamii.
Dkt. Mmbaga ametumia fursa ya kuhamasisha wananchi kufika kupata matibabu ya kibingwa ili kunusuru gharama kubwa za kwenda kutibiwa maeneo mengine nchini.
Katibu wa Itikadi mafunzo na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Uhagile ameipongeza serikali kwa kuleta huduma za kibingwa bobezi na kwamba ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020.
"Tunashuhudia serikali imewekeza miradi mbalimbali ya sekta ya afya na hii ya madaktari bingwa bobezi ni wamu pili kwa Hosptali ya Rufaa Mkoa na kuhamasisha jamii kutumia siku tano kufuata huduma" amesema.
Ofisa Uhusiano na Mawaliano, Aggrey Mwaijande amehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya afya.
No comments:
Post a Comment