Friday, March 29, 2024

UTAFITI: WATANZANIA WAUNGO MKONO MIKAKATI YA KUOUNGUZA UZALISHAJI WA METHANE KUSHUGHULIKIA MABADILIKO YA HAKI YA HEWA


 Na Esther Macha.

WATANZANIA wameonekana kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mipango inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane na kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa. 


Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Global Methane Hub, shirika la kibinadamu linalojitolea kupunguza uzalishaji wa methane duniani.

Utafiti huo, ambao ulijumuisha nchi 17 katika mabara sita, umetoa ufahamu wa jinsi jamii inavyoiona hali ya mazingira na njia za kisheria za kurekebisha hali hiyo na kuwa matokeo  ya utafiti huo yanaonesha kwamba asilimia 83 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sera zinazolenga kupunguza uzalishaji hatari wa methane, na kati yao, asilimia 49 wanatoa uungaji mkono mkubwa, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko nchi nyingine zilizofanyiwa utafiti.

POLISI KATA AWAREJESHA SHULE IRENE NA AGIZO

 

Polisi Kata ya Kinyala iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Lusajo Kibonde Machi 28, 2024 alifanikiwa kuwarejesha shuleni kuendelea na masomo wanafunzi wawili wa darasa la saba Irene Mwakwilusa na Agizo Anyimike.

Awali wanafunzi hao walikuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Ikukisya iliyopo Wilaya ya Rungwe lakini kutokana na changamoto mbalimbali na hali duni ya maisha waliacha Shule.

Machi 01, 2024 Polisi Kata ya Kinyala Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Lusajo Kibonde baada ya kupata taarifa za uwepo wa watoto hao, alilazimika kuitembelea familia hiyo na kufanya mazungumzo na mama mzazi wa watoto hao Bi. Christina Mwamengo.

Jitihada mbalimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja na kununua mahitaji ya Shule ya watoto hao na Machi 28, 2024 wamerejea shuleni na kuungana na wanafunzi wenzao kuendelea na masomo katika Shule ya Msingi Igembe iliyopo Wilaya ya Rungwe.


TUNAWATAKIA IJUMAA KUU NJEMA

 

Tunawatakia Ijumaa Kuu Njema. ⛪

Thursday, March 28, 2024

TIMIDA FYANDOMO KUMCHANGIA GODORO MJANE

Mbalaza wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Mbeya Timida Fyandomo ametembelea eneo la ujenzi wa nyumba ya muhitaji anayejengewa na taasisi ya Tulia Trust katika kata ya Iganjo Mbeya Mjini.

Akiwa katika eneo hilo Timida ameahidi kutoa Godoro kumsaidia muhitaji huyo ikiwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Tulia Trust chini ya Mkurugenzi wake ambaye ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Spika wa Bunge na  Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson.

Nyumba hiyo inayojengwa kupitia mpango wa Tulia Trust Mtaani Kwatu inatarajiwa kukabidhiwa kwa mlengwa huyo mapema mweezi Aprili mwaka huu.

Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema ujenzi wa nyumba hiyo iko katika hatua za mwishoni.

Amesema wanatarajia mara baada ya kukamilisha ujenzi huo uzinduzi utafanywa na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust.

DIWANI MATUNDASI AWAPA TABASAMU KWA WALIMU MSINGI NA SEKONDARI CHUNYA


Diwani Kata ya Matundasi Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Kimo Choga ameandika historia kwa  walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa kutoa motisha baada ya kuridhishwa na kupanda kwa ufauru  wa wanafunzi .

Choga amefanya tukio hilo jana katika hafla fupi aliyoandaa kwa kuwatanisha walimu, watumishi wa serikali viongozi na Chama cha Mapinduzi (CCM) sambamba na Madiwani kutoka baadhi ya Kata Wilaya ya Chunya.


Akizungumza walimu na watumishi wa serikali amesema kuwa amewiwa kutokaa ndani ya Moyo wake kufanya tukio hilo kwa kutambua mchango wa walimu katika kuchochea sekta ya elimu hususani kwa Shule ya Sekondari Makalla.

“Hili ni wazo nilikuwa nalo na nilishirikisha viongozi, wakuu wa shule, maofisa elimu kuwepo na mpango wa  kufanya tukio hilo kuona tunakaa kula pamoja na kubadilishana mawazo na walimu, kama Diwani matokeo mazuri ya sekta ya elimu yananipa sifa kubwa” amesema.

Wednesday, March 27, 2024

DKT. TULIA AHIMIZA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI NA KULINDA AMANI YA DUNIA

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wanachama wa Umoja huo kudumisha misingi ya IPU ikiwemo kuendeleza amani na usalama, kulinda misingi ya demokrasia, kuchagiza Mabunge jumuishi, kulinda usawa wa kijinsia na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akifunga rasmi Mkutano Mkuu wa 148 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Geneva (CICG), nchini Uswisi Machi 27, 2024.

Pia, amesisitiza Viongozi wa Mabunge wanachama kuona umuhimu wa kutoa taarifa za utekelezaji ndani ya Mabunge yao juu ya maazimio ya Mikutano Mikuu yanayopitishwa ili kuleta matokea chanya kwa jamii wanayoiwakilisha.

Vilevile amesema kuwa, IPU ni sehemu pekee ambayo Mabunge yanakutana kwa pamoja kupitisha maazimio yanayoihusu dunia na hivyo ni muhimu kwa Maspika wa Mabunge wanachama kuhudhuria Mikutano ya Umoja huo.

Mkutano wa 148 umehitimishwa rasmi jana huku ukiwa umehudhuriwa na takribani misafara ya Mabunge zaidi ya 145.


Tuesday, March 26, 2024

BODI YA NYAMA YAONYA WAUZAJI WA NYAMA WANAOPULIZA DAWA YENYE SUMU KWENYE MABUCHA

Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Nyanda za Juu Kusini imepiga marufuku wauzaji wa bucha za nyama kuachana na tabia ya kupuliza dawa zenye sumu ili kulinda afya za walaji.

Ofisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Mpoki Alinanuswe amesema jana mkoani hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kitendo cha wauzaji kupuliza sumu kunaweza kuleta madhara makubwa kwa walaji huku akibainisha watu 10 wamechukuliwa hatua katika Mikoa ya Mbeya na Songwe.

Monday, March 25, 2024

TULIA TRUST YATOA MIFUKO 400 YA SARUJI KUSAIDIA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

Taasisi ya Tulia Trust imechangia mifuko ya saruji 400 kwa Shule za Sekondari Dk Tulia Girls, Itende  sambamba na Shule ya msingi Mlimani iliyopo Kata ya Sinde Jijini Mbeya.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo amekabidhi mifuko hiyo leo na kuweka wazi ni utekelezaji wa ahadi ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo na Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini, Dkt. Tulia Ackson.

Mwakanolo ameagiza uongozi wa Shule hizo kusimamia kikamilifu saruji iliyotolewa itumike kwa malengo yaliyokusudiwa kuchochea sekta ya elimu.

MADEREVA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA YA BARABARANI

Madereva wa Magari ya mizigo, abiria na viongozi wametakiwa kuzingatia na kufuata sheria, alama, ishara na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 25, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga wakati akifungua mafunzo ya muda mfupi kwa madereva wa magari ya mizigo, abiria na viongozi katika Chuo cha udereva cha Agility Professional Driving School (APDS) cha Jijini Mbeya.

Pia, Kamanda Kuzaga amewataka madereva wanafunzi kuheshimu watumiaji wengine wa barabara kwani nao wana haki ya kutumia barabara.

MBUNGE MULUGO AOMBA SERIKALI KUJENGA SOKO LA MADINI

Mbunge wa Jimbo la Songwe Mkoa wa Songwe, Philipo Mulugo ameiomba Serikali kufungua soko la madini katika maeneo ya wachimaji wadogo ili kusaidia usalama mara baada ya kuchimba na kuingizwa sokoni kwa wakati.

Mulugo ametoa ombi hilo kwa Waziri wa Madini, Athon Mavunde aliyefanya ziara Wilaya jimboni kwake na kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo 19 kupitia Kikundi cha  Songwe Gold Family (SGF) kutoka  kata ya Saza wilayani humo

“Nipongeze Wizara ya kwa hatua hiyo licha ya Serikali kutoa leseni kuna kila sababu ya kujenga Ofisi ya Madini Wilaya ya Songwe Kata ya Saza ili kuwezesha ukunyaji wa  mapato ya biashara ya madini na  kuepusha utoroshaji

Naye Waziri Athon Mavunde amesema kwa kipindi cha mwaka Julai 2023 mpaka Februari 2024 zaidi ya kilo 729.6 zimeuzwa na kuingiza Sh 101.06 bilioni na utoaji wa leseni hizo itachangia ongezeko la mapato.

Mavunde amesema ili kuboresha wigo mpana katika sekta ya Madini Serikali imetangaza kufuta jumla ya leseni za maombi 2,648 ambazo hazijaendelezwa na kukiuka taratibu za umiliki.

Mwenyekiti wa Umoja wa wachimbaji Wilaya ya Songwe, Simon Ndaki amesema kitendo cha Serikali kuwapa leseni watajikita kuongeza nguvu katika uzalishaji ili kuchangia  mapato ya Serikali

DKT. TULIA AFUNGUA MKUTANO WA 148 WA IPU

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa 148 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha CICG, Geneva nchini Uswisi jana Machi 24, 2024.

Mkutano huo unatarajiwa kujadili Dhima Kuu ambayo ni “Matumizi ya Diplomasia ya Kibunge katika kuleta Amani na Maelewano Duniani”. Mkutano huo umehudhuriwa na Maspika wa Mabunge 48 na washiriki zaidi ya 1,500 na unatarajiwa kuhitimishwa Machi 27, 2024.

Huu unakuwa Mkutano wake wa kwanza kuufungua tangu achaguliwe kuwa Rais wa IPU katika Uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 nchini Angola.


Friday, March 22, 2024

MBEYA - UWSA YACHANGIA MABATI UJENZI SEKONDARI NA OFISI SERIKALI YA MTAA


Katika kilele cha kuadhimisha wiki ya Maji duniani Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYA - UWSA) imegusa jamii kwa kutoa msaada mabati bando nane kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

Msaada huo umetolewa kwa makundi mawili ikiwepo ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa Tonya Kata ya Ilomba na Kata ya Utengule Usongwe kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ihombe iliyopo jirani na chanzo cha Maji Ilunga.

Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Maji, Mhandisi Barnabas Konga amekabidhi msaada huo jana Machi 22 , mwaka huu katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Mamlaka hiyo.


BILIONI 11 ZABORESHA HUDUMA HOSPTALI YA RUFAA MKOA WA MBEYA

Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya Sh 11 bilioni kwa ajili ya kuboreshwaji miundombinu ya afya na kuchangia ongezeko la wagonjwa wanaofika kupata huduma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Machi 22 mwaka huu Mganga Mfawidhi Hosptali ya Rufaa Mkoa Dkt. Abdallah Mmbaga wakati akieleza mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema katika kuboreshwaji kwa huduma kati ya Sh 11 bilioni zilizotolewa na Serikali huku Sh 7 bilioni zimetumika kwa ajili ya mradi wa jengo la kisasa la upasuaji linaloweza kutoa huduma kwa wagonjwa sita kwa siku.

MWITIKO WA WANANCHI VITUO VYA AFYA KWAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO SONGWE

 Baadhi ya akina mama katika hospital ya Wilaya Songwe wakiwapeleka watoto kupata huduma za chanjo.

Na Baraka Messa, Songwe.

Mwitikio Mkubwa wa wananchi kutumia vituo vya afya hasa akina mama wajawazito na watoto mkoani Songwe kumepunguza vifo vya watoto wachanga na akina mama wakati wa kujifungua.

Hayo yamebainishwa na mganganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Boniface Kasululu alipofanya mahojiano na Mbeya Press Club Blog, baada ya kufanya kikao cha mikakati kuzuia vifo vya mama na mtoto hivi karibuni.

Alisema miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya akina mama wajawazito kuhudhuria klinik na kujifungulia kwa wakunga wa jadi, jambo lililokuwa linapelekea vifo vya Mama wakati wa kujifungua pamoja na watoto.

MAHUNDI AZINDUA UCHIMBAJI WA VISIMA VYA MAJI KATA TANO WILAYA YA MBARALI

Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Mhandisi Maryprisca Mahundi amezindua mradi wa uchimbaji visima vya maji uzinduzi uliofanyika Kijiji cha Azimio Mapula Kata Kongolo Mswiswi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ambapo Kata tano zitanufaika na mradi huo Wilaya ya Mbarali.

Mahundi amesema Wizara itakamilisha kiasi cha shilingi milioni 96 hivi karibuni kwa lengo la kuukamilisha mradi huo ili mitambo iweze kuhamie Kata zingine nao waonje keki ya Mama Samia Suluhu Hassan. Naibu waziri amesema visima vingine vitachimbwa katika vijiji vya Mpolo, Iwalanje, lbohola, Limsemi, Nyakazombe na Vikaye.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbarali Mhandisi Samwel Heche amesema mpaka sasa visima ishirini vimechimbwa Mkoani Mbeya tangu kuwasili mtambo huo Mkoani Mbeya na mradi wa Azimio Mapula ukikamilika utagharimu  shilingi 107,352,742/- mpaka sasa zimetumika  shilingi  10,400,000/- ili mradi ukamilike zinatakiwa shilingi 96,952,742 hivyo ameiomba Wizara kukamilisha fedha hiyo kukamilisha mradi.

MAMLAKA YA MAJI MBEYA KUTUMIA MIKUTANO YA HADHARA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya imeshiriki mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika he Kata ya Maanga.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Neema Stanton amesema lengo ni kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya maji, usomaji wa dira shirikishi, matumizi sahihi ya majisafi ili kuepuka ankara kubwa ya maji inayotoka na utumiaji wa maji isivyo sahihi.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutumia mfumo wa majitaka kwa usahihi kwa kuacha kutupa taka ngumu kwenye mfumo ambazo hupelekea mifumo ya majitaka kuziba na kuhatarisha afya za wananchi.

Pia Mamlaka imewataka wateja kutoa taarifa kwapale wanapokutana na changomoto ikiwepo watu wanaojihusisha kujiunganishia Maji kwa njia za kificho.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji, Mhandisi Barnabas Konga amesema kufuatia elimu inayotolewa ya wateja kuunganisha huduma hiyo mpaka sasa wamepokea maombi zaidi ya 700.

Thursday, March 21, 2024

TGDC: MRADI WA NGOZI KUANZA UZALISHAJI WA JOTO ARDHI MEGAWATI 30

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Mhandisi Methew Mwangomba amesema hatua hiyo imetokana na matokeo ya tafiti za wanasayansi kubaini uwepo wa kiwango kikubwa cha jotoardhi katika eneo hilo.

Mhandisi, Mwangomba amesema jana kwenye mkutano mkubwa wa wanasayansi kutoka mataifa mbalimbali ikiwepo Kenya. Mwangomba amesema lengo la kukutanisha wanasayansi wabobezi ni baada ya kupata matokeo mapya katika mradi wa Ngozi katika eneo la Magharibi na Kusini Mashariki .

"TGDC kwa kushirikiana na wanasayansi wabobezi kutoka mataifa mbalimbali na ukanda wa jotoardhi Afrika ikiwepo Kenya, Rwanda, Ethiopia tutajadiliana kuona namna bora itakayowezesha kuanza  uchimbaji wa rasirimali hiyo pasipo kuathiri mazingira" amesema Mwangomba.

Mwangomba amesema tafiti za kisayansi zimeonyesha uwepo wa rasirimali ya ya jotoardhi katika eneo la mradi wa Ngozi na  kubainisha kuanza kuchimba mita 1200 ili kukutana na kiwango cha  joto 250.

MJANE APEWA TABASAMU NA TAASISI YA TULIA TRUST

Mjane Sigwava Jackson (60) amemshukuru Mbunge wa Mbeya mjini, Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia kwa kumtupia jicho na kumjengea makazi bora.

Sigwava Mkazi wa mtaa Itanji Kata ya Iganjo Jijini Mbeya amepata tabasamu hilo baada ya Taasisi ya Tulia kupitia mpango wa Tulia Trust mtaani kuboa makazi ya awali ambayo yalikuwa hatarishi na kumjengea nyumba ya kisasa.

Mjane huyo ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba  iliyoezekwa maturubai yeye na watoto wake sita huku wakipitia changamoto za ya namna ya kuendesha maisha kila siku ya kujikwamua kiuchumi.

Wednesday, March 20, 2024

TBL, MBEYA - UWSA, RUWASA, WAPAMBA WIKI YA MAJI KWA KUPANDA MITI 3,000

 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYA - UWSA) kwa kushirikiana na Kampuni ya bia (TBL) wamepanda miti 3,000 katika chanzo cha maji cha Mwatezi kilichopo Uyole Jiji Mbeya kwa lengo la kuhimiza utunzaji wa mazingira.

Lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha huduma ya maji inakuwa bora na endelevu katika jamii kwa kutunza vyanzo vya maji.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka Neema Stanton  ameonya wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya Maji kwani vinachangia upotevu wa Maji kwa kiwango kikubwa.

AFISA TARAFA AKERWA NA WATENDAJI WAZEMBE

Afisa Tarafa ya Ilongo Magdalena Sikwese ameagiza Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha wanatumia nafasi zao kwa kuwatumikia Wananchi vizuri ikiwemo kuwa na kauli nzuri, kuwa wakarimu, kusoma mapato kwa wananchi, kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.


"Watendaji tumeshau wajibu wetu wa kusoma mapato na matumizi. Sisi Watendaji tumefika kwenye maeneo ya Wananchi tukajifanya nasisi wananchi, tumesahau kwamba hao Wananchi tumewafahamu baada ya kupata ajira hapo." 

Sikwese amesema unaposoma taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi inatia moyo hata utakapowaomba michango mingine ya kimaendeleo itakuwa rahisi kujitoa.
Pia Sikwese amesema kila mtu akitimiza wajibu wake ipasavyo, basi Tarafa ya Ilongo itakuwa na maendeleo huku akikemea tabia ya baadhi ya Watendaji kuwajibu vibaya Wananchi pale wanapohitaji huduma kutoka kwao.

MADIWANI MBEYA WAVUTIWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI

Madiwani viti maalum Jiji la Mbeya wamesema wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Maji iliyosimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBEYA - UWSA).

Kauli hizo wametoa Jumanne Machi 19, mwaka huu baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi wa Ilungu Wilaya ya Mbeya vijijini uliogharimu Sh 4.8 bilioni na mradi wa Itagano na Mwansekwa yenye thamani ya Sh 5.2 bilioni.

Diwani viti maalum Attu Msai na Mjumbe wa bodi ya Maji mesema miradi hiyo imekuwa mkombozi mkubwa  kwa wananchi kwani walikuwa na  adha kubwa kwa kipindi kirefu.

Tuesday, March 19, 2024

WATU 10 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUTOROSHA KILO 9.5 ZA DHAHABU

Wafanyabiashara 10 wa madini wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya kwa tuhuma za kutorosha kilo 9.5 za madini ya dhahabu.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema thamani ya dhahabu iliyokamatwa ina thamani ya shilingi bilioni 1.5 ambapo watu kumi wanahusishwa na tukio hilo Ilomba Jijini Mbeya.

Mavunde amesema tukio hili ni la pili kutokea Mkoani Mbeya na kuagiza kamishina wa madini kuzifuta leseni zote zinazomilikwa na watu hao pamoja na leseni zote zinazomilikea na watu hao nje ya Mkoa wa Mbeya.

MBEYA KUONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAJI MACHI 2025

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (MBEYA - UWSA) imesema mradi mkubwa wa kimkakati wa chanzo cha mto Kiwira Wilayani ya Rungwe utakamilika ifikapo mwezi Machi 2025.

Mradi huo utakaogharimu Sh 250 bilioni mpaka kukamilika ambapo katika awamu ya kwanza zitatumika Sh 119 bilioni katika hatua mbalimbali ikiwepo usanifu na ujenzi huku ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 117.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mhandisi Barnabas Konga amesema, Jana mara baada ya kutembelea eneo la utekelezaji wa mradi huo wilayani Rungwe, ikiwa ni sehemu ya kuelekea wiki ya Maji Duniani ambayo iliyoanza Machi 16 mpaka 22 mwaka huu.

Monday, March 18, 2024

WAZIRI MKUU KUFUNGUA KONGAMANO LA IDHAA ZA KISWAHILI JIJINI MBEYA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa Majaliwa amewasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe uliopo Mkoani Mbeya na kupokelewa na Mwenyeji wake Juma Homera Mkuu wa Mkoa wa Mbeya

Mh. Majaliwa amewasili mkoani huo kwaajili ya kufungua Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani linalofanyika kuanzia leo March 18 - 22, 2024 katika Ukumbi wa Eden Highlands Hotel, Jijini Mbeya.