Monday, August 12, 2024

DKT. NCHIMBI AAGIZA VIONGOZI WA CHADEMA, WAANDISHI WA HABARI WAACHIWE HURU


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuzungumza na waziri wake, Hamad Masauni, kuwaachia huru viongozi wa Chadema waliokamatwa na Polisi mkoani Mbeya.

Dkt. Nchimbi amesema hayo leo Agosti 12, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Katoro iliyopo mkoani Geita anakoendelea na ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema alifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wenzake wa vyama vingine vya siasa, ili wawe na mazungumzo kama vyama vya siasa, aliwasiliana na baadhi ya makatibu wakuu, hata hivyo alipata taarifa wengine wamekamatwa mkoani Mbeya.

“Kwakuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani upo hapa, mambo ya sheria sio ya kutolea maelekezo Kiongozi wa Chama cha siasa lakini nitumie nafasi hii mwambie Waziri wako (Hamad Masauni) kwamba tunaomba muone uwezekano wale Viongozi wa Vyama vya siasa waachiliwe ili mtupe nafasi ya kuzungumza nao kwasababu tunajenga Taifa moja tunapenda kuwa na Taifa tulivu kama kuna maeneo wamekosea wao au tumekosea sisi tukae tuzungumze tuijenge Nchi yetu” Dkt. Nchimbi.

Baadhi ya viongozi wa Chadema wanaodaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi ni Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lisu, Katibu Mkuu John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi (Sugu), Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), John Pambalu na viongozi wengine.

Pia waandishi wa habari Ramadhan Khamis na Fadhil Kirundwa wote wa Jambo TV na Francis Simba mpiga picha wa Mwanzo TV nao wanashikiliwa na jeshi hilo.

No comments:

Post a Comment