Tuesday, August 6, 2024

DKT. TULIA WANANCHI TOENI TAARIFA ZA WAOMBA RUSHWA WASHUGHULIKIWE

Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amewataka wananchi jijini hapa kutoa taarifa za siri za viongozi wanaoshawishi kutoa Rushwa wakati wakihitaji huduma.

Dkt. Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ametoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Ofisi za CCM kata ya Kalobe Jijini hapa.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya mmoja wa wakazi wa kata hilo kueleza kuwepo kwa baadhi ya viongozi kutaka rushwa pindi wanapokwenda kuhitaji huduma.

Kufuatia malalamiko hayo Dkt. Tulia amesema Rushwa haikubailiki na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji endapo kama wataona kumfikia yeye ni changamoto.

Wakati huo huo Dkt. Tula amesema Serikali imepiga vita vitendo vya rushwa na kwamba hawataki wananchi kunyanyasika pasipo sababu.

Hata hivyo ameonya walioanza kupita mitaani kupiga kelele na kwamba Mbeya ni shwari wanaotaka waje wasiangalia wembamba wa reli waangalie uzito wa behewa.

"Tumejipanga mwakani tuko vizuri tutawavuruga na msimu huu tunaelekea uchaguzi wa serikali za mitaa niiwatake wananchi mpuuze vijembe na kuwa puuza hao wanaopita kuwarubuni" amesema.

Dkt. Tulia amesema kwa sasa hana mpango wa kuacha jimbo la Mbeya mjini na wataendelea kuisemea serikali kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naye Diwani wa Kata ya Kalobe Ally Bromela amesema wameona jitihada za Mbunge huyo hususani katika sekta ya elimu ikiwepo madawati na matundu ya vyoo.

Sambamba na hilo ameomba serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wa mfereji wa kilimo cha umwagiliaji.

Mkazi wa Kalobe Aswile John amesema wamejipanga kuhakikisha Dkt. Tulia anarejea kwa kishindo na hawatafanya makosa kurejea miaka 10 iliyopita.

No comments:

Post a Comment