Monday, August 12, 2024

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUANDIKA HABARI ZA KUISAIDIA JAMII

Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuandika habari zitakazosaidia kutatua kero za wananchi kwa kuwa habari hizo zitasaidia kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya habari.

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC) Keneth Simbaya, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo.

Simbaya alisema kwa miaka ya karibuni imani ya wananchi kwenye vyombo vya habari imeshuka kutokana na waandishi wa habari kuripoti habari ambazo hazina tija kwao.


Alizitaka klabu za waandishi wa habari kutumia vyombo vyake zikiwamo televisheni za mtandaoni kuandika habari za wananchi kwa madai kuwa kwa sasa imani ya wananchi imebaki kwenye klabu hizo.

"Nawaomba sana waandishi wa habari tuandike habari ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja, wananchi wanataka habari ambazo zinatatua kero zao, wananchi wanahitaji habari ambazo zinatatua kero za maji, barabara na shida zao zingine," alisema Simbaya.

 Hata hivyo alisema Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (MBPC) ni miongoni mwa vyama ambavyo vina maendeleo mazuri ikiwamo uendeshaji wa kikundi cha kuweka na kukopa (VICOBA) na kuwa mfano kwa nchi nzima.

Aliwataka viongozi wa MBPC kuendelea kuwaunganisha waandishi wa habari wa mkoa huo ili kuwa na nguvu zaidi akidai kuwa vyama vya waandishi wa habari vya mikoa vikiwa imara vinasababisha hata UTPC kuwa imara zaidi.

Mwenyekiti wa MBPC, Nebart Msokwa alisema mpaka sasa chama hicho kina wanachama 70 na wanne ambao ni wanachama wa heshima.


Alisema kati ya wanachama hao, 40 wamejiunga kwenye VICOBA ambayo ni moja kati ya njia za kuwainua wanahabari kiuchumi na kuondokana na tatizo la umaskini ambalo limekuwa likiwakabili.

"Kupitia VICOBA wanachama wanakopeshana fedha ambazo wanazitumia kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo ujenzi wa nyuma, kusomesha watoto na hata kuanzisha biashara," alisema Msokwa.

Mwenyekiti wa Mbeya Press VICOBA, Ezekiel Kamanga, alisema mpaka sasa chama hicho kina zaidi ya Sh. milioni 38 ambazo ni hisa za wanachama na kwamba mzunguko wa mikopo ni zaidi ya Sh. milioni 58.


No comments:

Post a Comment