Tuesday, August 6, 2024

MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BIMA (TIRA) YAANZA ZIARA MKOA WA SONGWE


Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA) imeanza ziara kuwatembelea Wakuu wote wa Mikoa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo kuitambulisha Mamlaka na utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayotekelezwa nchini.

Ziara hiyo inaongozwa na Kamishina wa Bima nchini Dkt Baghayo Saqware akiambatana na wataalam katika vitengo mbalimbali na Viongozi wa Kanda.

Akiwa Mkoa Songwe mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo, Dkt. Baghayo Saqware amesema lengo la Mamlaka ni kuwahamasisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya afya kwa wote pili kutambulisha ofisi za Mamlaka za Kanda pamoja na majukumu ya Mamlaka kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya tatu kutoa elimu ya bima kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili waweze kuwa mabalozi kwa wananchi wanaowasimamia kwa kuwahamasisha kutumia bidhaa na huduma za bima.


Dkt. Saqware amesema Mamlaka imeendelea kukua kwa kasi ya asilimia kumi na tano na wananchi wamekuwa wakinufaika na huduma za bima kwa asilimia tisini na tano nchini.

Aidha Mamlaka imeendelea kuwasimamia watoa huduma za bima ili kuhakikisha wanatoa  huduma kwa ubora zikiwemo bima za afya,nyumba na magari.

Amesema hivi sasa Mamlaka inahakikisha malipo yanafanyika kwa haraka zaidi ili kuwaondolea kadhia wananchi kutoka kwa watoa huduma za bima nchini.

Saqware amesema hivi sasa wanawasiliana na LATRA Ili tiketi zinazotolewa na mabasi zioneshe wakala wa Bima ili kuondoa urasimu pindi abiria anapopata ajali.

"Leo tunajitambulisha Mkoa wa Songwe kwa kuwa ni Mkoa unaopitisha bidhaa nyingi zinazosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi za Kusini mwa Afrika" alisema Dkt. Saqware.

Dkt Saqware ameomba ushirikiano baina ya Serikali ya Mkoa wa Songwe ili elimu iwafikie wananchi sanjari na ombi la kuipeleka sera hii ili iingizwe kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Samwel Mwiku Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Uendelezaji Soko Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) amesema utafiti unaonesha kuwepo kwa ongezeko la wananchi kuona umuhimu wa matumizi ya huduma za bima ambapo elimu ikiendelea kutolewa itaongeza kasi ya matumizi ya bima ikiwemo ya afya na mali.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo amefurashwa zaidi na majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini TIRA kwa Mkoa wa Songwe ni lango la uchumi nchini kutokana na bidhaa nyingi kupitia mpaka wa Tunduma.

Aidha Chongolo ameshauri wananchi kutumia huduma za bima zikiwemo za majengo na magari ya Serikali ambayo hayakatiwi bima.

"Inashangaza mtu amejenga nyumba yenye thamani kubwa lakini anashindwa kulipa bima ya shilingi laki moja na elfu hamsini tu wakati jengo lake limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja"alisema Chongolo.

Chongolo ameomba TIRA kuendelea kutoa elimu kwa madereva wa Bodaboda kwa kuwa ni watumisji wakubwa wa vyombo vya moto na wao ni waathirika wakubwa wa ajali.

Kwa upande wake Neema Lutula Meneja wa Kanda ya Nyanda za juu TIRA ikijumuisha mikoa ya Mbeya, Njombe na Songwe amesema elimu imeendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali Mkoa wa Songwe ambapo hivi karibuni wametoa elimu kwa madereva wa Bodaboda Tunduma na madereva zaidi ya mia moja wamefikiwa na elimu pia wamekata bima.

Amesema  wataendelea kuyafikia makundi mbalimbali katika Mikoa ya Mbeya, Njombe na Songwe ili wananchi waone umuhimu wa matumizi ya bima mbalimbali.

Ziara hiyo itaendelea katika Wilaya zote za Mkoa wa Songwe ambazo ni Mbozi, Songwe, Momba na Ileje.

No comments:

Post a Comment