Wednesday, August 7, 2024

BILIONI 117 KUTEKELEZA MRADI WA MAJI MTO KIWIRA, MBEYA

Serikali imetoa zaidi ya Sh Bilioni 117 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati kutoka chanzo cha maji cha mto kiwira ambao unatarajia kukamilika Aprili 31 mwakani.

Mbunge wa Mbeya mjini  Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson amesema leo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji katika kata za Mwansekwa, Itagano na Ujenzi wa tenki kubwa  lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 70 kwa siku.

Dkt. Tulia amesema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kutekeleza sera ya maji kwa vitendo sambamba na wananchi linapopita bomba la mradi wa mto Kiwira kunufaika na mradi huo ili kutunza miundombinu.


Pia akiwa katika mradi wa Maji kata za Itagano na Mwansekwa ametaka iwekwe mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi kulima mazao ya muda mrefu kwenye maeneo ya safu za milima ili kutunza vyanzo vya maji.

Amesema kwa sasa asilimia 90 ya wananchi wanapata maji huku kukiwa na jitihada za makusudi kuhakikisha asilimia 100 wanapata huduma bora na salama.

"Nipongeze uongozi wa Mamlaka ya Maji Mbeya mnafanya kazi kubwa sana kuhakikisha mnasimamia utekelezaji wa miradi sambamba na ongezeko la mapato kutoka milioni 80 mpaka bilioni 1.4 ya mapato ya ndani".


Naye Mkurugenzi mtendaji Mhandisi Gabriel Kayange ameishukuru serikali kwa kuwekeza mradi mkubwa wa kimkakati kutoka chanzo cha mto Kiwira ambao utakuwa suruhisho la hadha ya maji.

Mwenyekiti wa Bodi amesema wana kila sababu kupongeza jitihada za Mbunge wao na Spika wa Bunge Dkt. Tulia kwa kufanya msukumu wa uwekezaji wa mradi huo.

No comments:

Post a Comment