Tuesday, August 6, 2024

RAS KILIMANJARO AWATAKA WAANDISHI KUCHAGIZA MAENDELEO

 Serikali mkoani Kilimanjaro imewataka waandishi wa habari mkoani humo kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali katika kuchagiza  maendeleo ya mkoa huo kwa kuwa vyombo vya habari vinayo nafasi kubwa ya kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana mkoani humo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS) Kiseo Yusuph Nzowa amesema hayo wakati akimkaribisha Balozi wa Sweden Mh. Charlotta Ozaki alipotembelea Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kilimanjaro (MECKI).

Nzowa amewapongeza waandishi wa habari mkoani humo kwa kuandika habari chanya zinazochochea maendeleo ya mkoa huo.

Amsema serikali itaendelea kushirikiana na vyombo hivyo vya habari na kuhakikisha waaandishi wa habari wanafanya kazi zenye kuleta tija katika jamii na serikali kwa ujumla.

"Tunawashukuru waandishi wa habari wa mko huu wa Kilimanjaro kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanyakazi kwa karibu na serikali yetu ya mkoa na kuhakikisha wanatangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana hapa Kilimanjaro" amesema Nzowa.

Balozi Ozaki amesema suala uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza umekuwa ndio uti wa mgongo wa mahusiano mazuri baina ya Tanzania na Sweeden,ushirikiano baina ya nchi hizi ulianza toka Tanzania ilipopata uhuru wake.

Amesisitiza kuwa, uhuru wa kujieleza ni eneo muhimu linaloungwa mkono na Ubalozi wa Sweeden ili kuboresha uhuru wa vyombo vya habari. Amefurahishwa na mahusiano mazuri yaliyopo baina serikali mkoani Kilimanjaro na waandishi wa habari mkoani humo.

No comments:

Post a Comment