Sunday, August 4, 2024

WAKULIMA WA NDIZI RUNGWE WATAKA VIWANDA KUONGEZA THAMANI MAZAO

Wakulima wa zao la ndizi na parachichi Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya wameeleza ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani mazao  imekuwa mwiba kwao kujikwamua kiuchumi.

Wamesema hali hiyo imekuwa ikipelekea kuzalisha kwa wingi mazao ya kimkakati kwa wingi huku changamoto ni ukosefu wa masoko ya uhakika hususani kwa zao la parachichi na kupelekea kuharibikia mashambani.

Mkulima Byaison Mbungula akizungumza na mwandishi wetu jana Jumapili Agosti 4, 2024  kwenye banda la  maonyesho ya sikukuuya wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale ambayo kikanda yanafanyika Mkoa wa Mbeya.

"Zipo bidhaa mbalimbali ambazo zinaweza kuzalishwa kwa mazao ya parachichi ikiwepo mafuta ya kupakaa, sabuni ambapo vikiwepo viwanda wakulima tutajikwamua kiuchumi" amesema.

Amesema kuwa ukifika msimu wa mavuno wakulima ujikuta kuzalisha kwa wingi lakini uhakika wa soko ukawa mdogo hali ambayo inasababisha kupata hasara kwa kuuza kwa bei ya chini na hata mazao mengine kuharibika.

"Kilio chetu kikubwa ni viwanda vya kuchakata mazao tunayolima ili tuweze kuzalisha kwa tija na kupata faida na kama serikali imeshindwa basi itafute wawekezaji kuja kuwekeza Wilaya ya Rungwe" amesema.

Ametoa mfano, unakuta wakulima tunazilamika kuuza parachichi kwa kilo moja Sh 1,500 badala ya bei elekezi ya serikali ya Sh 1,700 na hivyo kuendelea kudidimia kiuchumi.

Kwa upande wake msindikaji wa mazao ya mbogamboga, ndizi na parachichi, Joyce Mkumbwa amesema kutokana na ukosefu wa masoko ya mazao wanayozalisha ameona njia mbadala ni kuyaongezea thamani.

"Unajua Rungwe ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya kimkakati mbali na ukosefu wa masoko tunashukuru Halmashauri imekuwa na mkakati wa kutoa elimu ya ujasiriamali usindikaji wa mazao ili kuepuka hasara na badala yake kupata faida" amesema.

Ametaja faida za kusindika mazao ni kuongeza ubora na viwango vya hali ya juu hususani kuwepo kwa soko la uhakika huku akiomba serikali kuwajengea uwezo utakao kuwa chachu ya kuongeza ubunifu.

Awali akizungumza na Mwananchi Digital kwenye banda la maonyesho la Wilaya ya Rungwe, Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Agustino Lawi amesema Halmashauri iko kwenye mchakato wa kujenga miundombinu ya ghara la baridi kwa ajili ya kuhifadhia mazao.

Amesema tayari wametenga eneo lenye ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kuhifadhi mazao ili yasiharibike.

"Kwa sasa mazao yanahifadhiwa kwenye miundombuni ya baridi Mkoa wa Njombe hali ambayo inamsababishia mkulima kutumia gharama kubwa ya usafishaji na utunzaji" amesema.

Lawi amesema kama Wilaya wanaendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza viwanda vya kuchakata mazao yanayozalishwa ili kuwasaidia wakulima kuondokana na hasara zinazojitokeza.


No comments:

Post a Comment