Wednesday, October 16, 2024

MILIONI 15 KUTUMIKA UJENZI SOKO LA MBOGA MBOGA KATA YA ISANGA

Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeanza utekelezaji wa Ujenzi wa mradi wa soko la kisasa la  mbogamboga katika Kata ya Isanga.

Mradi huo kwa awamu ya kwanza umegharimu Tsh. 15 milioni na litakapo kamilika litakuwa fursa kwa wakulima wa mbogamboga kujikwamua kiuchumu na kuongeza wigo wa masoko ya ndani na nje.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa amesema leo Oktoba 16 mwaka huu na kwamba ujenzi wa soko hilo ni sehemu ya miradi ambayo imepokelewa katika Kata ya Isanga.

"Ujenzi wa soko la mbogamboga la Isanga utekelezaji wake umeanza na uko katika hatua nzuri sambamba na miradi mingine ya uboreshwaji wa barabara na kufunga taa" amesema Issa.

Tuesday, October 15, 2024

MBUNGE WA LUPA ALIA NA TRA UTITIRI WA KODI WACHIMBAJI WADOGO

Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Masache Kasaka ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza utitiri wa tozo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

Masache amesema Oktoka 14 ikiwa ni usiku wa madini ambayo Mkoa wa Mkuu wa Mkoa Juma Homera alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Madini Athon Mavunde.

"Tukuombe Mkuu wa Mkoa tuwasilishie kilio chetu kwa Waziri mwenye dhamana kutazama changamoto ya cha utitiri wa tozo kwa wachimbaji wadogo ili kuwezesha kuendesha shughuli zao na kutokwepa kulipa kodi" ameseme Masache.

RAIS WA UTPC AKIJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA


Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo, amejiandikisha katika daftari la wakazi katika kitongoji cha Kabatini kijiji cha Isinde katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.


Nsokolo ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka watakaosaidia kuleta maendeleo katika maeneo yao.

MEYA MBEYA AHAMASISHA WANANCHI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA


Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa amehamasisha wananchi na vyama vya siasa kusimamisha wagombea kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Issa ambaye ni Diwani wa Kata ya Isanga mesema leo Oktoba 14, 2024 mara baada ya kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura kwenye mtaa wa Ilolo Kata ya Isanga Jijini hapa.

Amesema kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kushiriki kuanzia zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa kuanzia hatua uandikishaji katika dafrari la wapigakura.

Thursday, October 10, 2024

AGRICON BORESHA CHAI YANUFAISHA WAKULIMA MBEYA, NJOMBE, IRINGA

 

Wakulima zaidi ya  22,000 Mikoa ya Mbeya,Njombe na Iringa wamenufaika na  mafunzo ya shamba darasa kupitia mradi  Agricon Boresha  Chai uliotekelezwa na Shirika la IDH Tanzania kwa ufadhiri wa Jumuiya ya Ulaya (EU)

Meneja mradi wa Shirika hilo  ,Elikinda Tenga amesema  jana Oktoba 9,2924  wakati  wa  Mahafari ya  Mafunzo ya  Wakulima ya Shamba  Darasa(FFS)  yaliyofanyika katika kijiji cha Syukula Kata ya Kyimo Wilaya ya Rungwe

Amesema  mradi wa Agricon Boresha chai umelenga kuwajengea uwezo wakulima na kuwezesha upatikanaji wa  vifaa vya kisasa na matumizi ya teknolojia kutumia matone kunyunyiza kwenye mashamba.

MAWAKALA VYAMA VYA SIASA WAAPISHWA JIJI lA MBEYA

Halmashauri ya Jiji la Mbeya limewaapisha mawakala wa vyama vya siasa leo  Oktoba 10, 2024 katika ukumbi wa Mkapa Jijini hapa.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Teddy Mlimba amewaapisha mawakala hao huku  viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakishiriki na kutoa maoni yao kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.

Ofisa uchaguzi Jiji la Mbeya Gregory Emmanuel amesema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu utakuwa wa huru na kuzingatia demokrasia ya mifumo ya vyama vingi.

Tuesday, October 8, 2024

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI WAAPISHWA WAONYWA MATUMIZI YA POMBE

 Halmashauri ya Jiji la Mbeya leo Oktoba 8, 2024 imefanya zoezi la kuwaapisha wasimamizi wa uchaguzi zaidi ya 200 ngazi za mitaa katika kuelekea zoezi la uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la wapigaku.

Zoezi hilo limefanyika katika Ukumbi wa Mkapa Jijini hapa kwa  kula kiapo mbele ya Hakimu wa Mahakama wa Wilaya Mkoa wa Mbeya .

Awali akizungumza baada ya kuapishwa, Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jiji la Mbeya Oddo Nduguru amewaonya wasimamizi kuepuka matumizi ya vilevi wakati wa kuendesha zoezi hilo ili kutunza siri za kiapo walichopewa.

"Tunaelekea zoezi la Uandikishaji Daftari la kudumu la wapigakura litakaloanza Oktoba 11 mpaka 20 mwaka huu kwa wale wanatumia vilevi tunaomba wakawe wavumilivu kwa siku 10 za kuendesha zoezi hilo" amesema.

UJENZI MRADI WA MAJI MTO KIWIRA WAFIKIA ASILIMIA 35

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya umefikia asilimia 35 ambao unatarajia kunufaisha watu zaidi milioni 1.4.

Mkurugenzi uzalishaji na usambazaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya (MBEYA - UWSA) Mhandisi Barnabas Konga amesema jana wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kapudi.

Mradi huo utajengwa kwa miaka miwili ambapo ukikamilika utazalisha lita milioni 184 kwa siku na wananchi zaidi ya milioni 1.4 katika Mkoa wa Mbeya na Mji wa Mbalizi watanufaika kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

Monday, October 7, 2024

PROF. KABUDI AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI WA BILIONI 4.8 MBEYA

Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Ilungu Kata ya Utengule Usongwe Wilaya ya Mbeya.

Mradi huo una thamani ya zaidi ya Sh 4.8 bilioni na kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya-UWSA) ambao unatarajia kunufaisha wananchi 110,000 kutoka vijiji vitatu na kata nne.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ihango kata ya Utengule Usongwe Prof. Kabudi ameeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wanaondokana na changamoto ya maji.

"Nipongeze sana Mamlaka ya Maji Mbeya kwa kutekeleza mradi huu mkubwa ambao unakwenda kuwa mwarobaini kwa wananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa wakati" amesema Prof. Kabudi.

Friday, October 4, 2024

NCHIMBI AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUHAMASISHA WAUMINI KUPIGA KURA

Msimamizi wa Uchaguzi Mdogo wa Serikali za mitaa Jiji la Mbeya John Nchimbi amewaomba viongozi wa dini,machifu kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki  katika uchaguzi Novemba 27, 2024 kuchagua viongozi bora.

Nchimbi amesema leo Ijumaa Oktoba 4, 2024 kwenye kikao kilichohusisha viongozi wa dini,machifu wadau na viongozi wa vyama siasa kilicholenga kutoa maelekezo kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa.

Nchimbi amesema kuwa mchakato wa kuelekea uchaguzi umekamilika hivyo wananchi wajitokeze kushiriki kikamilifu hususani kujiandisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni wajibu wao wa kikatiba.

Thursday, October 3, 2024

MEYA ISSA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA TACTIC

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa leo amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Soko la Kisasa la Matola  na mitaro ya kutililisha Maji ya Mvua  katika Kata ya Nzovwe.

Miradi hiyo inatekelezwa kupitia Mradi wa kuboresha majiji (TACTIC) ambayo iko katika hatua nzuri za utekelezaji.


Akizungumza na Mwandishi wa habari leo mara baada ya kufanya ziara hiyo, Issa ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Sami Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mikubwa ya kimkakati Jijini hapa.

"Kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Mbeya mjini, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson wanaona Mkoa wa Mbeya unakwenda kasi katika miradi ya maendeleo" amesema Issa.


Amesema amekuwa Meya wa IPU kwani miradi inatekelezwa kwa kasi ukiachia ujenzi wa soko na mifereji pia kuna ujenzi wa kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi ya mikoani ambacho kitakuwa chachu ya fursa za kiuchumi na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi.

MKUTANO WA MWAKA WA WAKUU WA MAMLAKA ZA KUPAMBANA NA RUSHWA KWA NCHI ZA SADC 2024 - LUSAKA, ZAMBIA

Wakati Dunia ikishuhudia majanga katika maeneo mbalimbali, Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC zimetahadharishwa kuwa makini kwani mikakati ya haraka inayoandaliwa kukabiliana na hali hiyo inaweza kutoa mianya ya rushwa.
 
Akizungumza Oktoba 2, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa mamlaka hizo jijini Lusaka - Zambia, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya SADC ya Kupambana na Rushwa (SADC Anti Corruption Committee - SACC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini - TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, amefafanua kuwa hatari ya uwepo wa vitendo vya rushwa inaweza kujitokeza wakati wa mchakato wa kupata na au kutoa misaada wakati wa dharura. 

“Hatua zote za mnyororo wa utoaji wa misaada ziko katika hatari ya rushwa kutokana na dharura inayokuwepo", alisema.


Wakuu wa Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC pamoja na Viongozi na wajumbe mbalimbali kutoka katika mamlaka hizo za Nchi 14 wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Tuesday, October 1, 2024

MBUNGE MASACHE AZINDUA MASHINDANO AMBWENE CUP

Mbunge wa Jimbo la Lupa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya Masache Kasaka amezindua mashindano ya Ambene Cup 2024 yanayotimua kivumbi katika viwanja vya Matundasi "A".

Mashindano hayo yatashirikisha timu 32 huku yakifunguliwa na timu ya Chokaa FC na kisimani FC zote za wilayani Chunya katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Imeelezwa timu zitakazo ibuka kidedea zitajinyakulia kitita cha fedha huku  mbalimba mshindi wa kwanza  Sh 5 milioni wa pili Sh 3 milioni wa tatu Sh 2 milioni huku wa nne shilingi milioni moja.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mashindano hayo Masache ametaka ukawe wa haki bila kupendelea upande wowote na vijana kutumia kama fursa ya ajira na kiuchumi.


BODOBODA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA BARABARANI

Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini ambaye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson amezindua Jengo la Ofisi ya Bodaboda Kanda ya Soweto Mbeya Mjini huku akisisitiza kutii sheria za usalama barabarani.

Ofisi hiyo imejengwa katika Mtaa wa James Kata ya Ilemi kwa Jitihada za Wanachama wa Bodaboda Kanda ya Soweto ili iwasaidie katika Shughuli mbalimbali za Kiofisi na kuwaongezea kipato kupitia Vyumba vya Biashara vilivyojengwa kwenye Ofisi hiyo.

Dkt. Tulia amewaasa Madereva Bodaboda kufuata Sheria za Usalama Barabarani na kutumia vizuri vyombo vyao vya Moto katika kujitafutia kipato na sio uhalifu ili kutimiza Malengo yao kama ambavyo wamefanikisha kujenga Ofisi hiyo.

Aidha Dkt. Tulia amewataka Wananchi  wajitokeza kujiandisha kwenye Daftari la Mpiga Kura ili waweze kutimiza haki yao ya kupiga kura kuwachagua Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Uchaguzi Utakaofanyika Mwezi Oktoba Mwaka huu.


DKT. TULIA ACHANGIA MIFUKO 100 YA SARUJI KWAAJILI YA UJENZI WA OFISI YA SERIKALI YA MTAA

Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya serikali ya Mtaa Kata ya Isanga Jijini hapa.

Mbali na kuchangia ujenzi huo pia amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa zahanati ya kata hiyo sambamba na  kufungua ofisi ya bodaboda  eneo la Ilemi Jijini hapa.

Akizungumza na mamia ya wananchi leo Oktoba mosi Dkt. Tulia amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha miradi ya maendeleo kama kutekeleza ilani ya uchaguzi 2024/25.

Amesema pia serikali imewekeza zaidi ya Sh 11 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hosptali ya Rufaa Kanda kitengo cha Wazazi Meta.

Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya na Diwani wa kata ya Isanga Dour mohamed Issa amesema  kwa kipindi cha uongozi wa  Dkt. Tulia wamepata miradi mbalimbali kama miundombinu ya barabara, zahanati.

"Tuna kila sababu ya kujivunia uwepo wa Mbunge Dkt. Tulia tumepokea miradi mbalimbali ambayo imekuwa mwarobaini na tija kubwa kwa  wananchi".


Mkazi wa Isanga Stella Joel ameomba serikali kuharakishwa ujenzi wa zahanati ya kata ili kuokoa wakinamama wajawazito kutembea umbali mrefu kufuata huduma.