Monday, July 15, 2024

TANROADS MBIONI KUANZA UJENZI BARABARA YA MBALIZI - SHIGAMBA

Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya umesema unatarajia kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha rami kutoka Mbalizi hadi Shigamba na Umalila baada ya serikali kutoa bilioni 2.

Kaimu Meneja, TANROADS Mkoa wa Mbeya Mhandisi, Kamokene Sanke amesema leo Jumamosi Julai 13, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sanje kata ya Santilya wilayani Mbeya kwenye ziara ya Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Manasse Njeza ya kusikiliza kero za wananchi.

Amesema Serikali Kuu chini Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Sh 2 bilioni  kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha rami kutoka Mbalizi mpaka Shigamba yenye urefu wa Km 52 ambayo inatarajia kuanza hivi karibuni.

Kaimu Meneja Wakala wa Barabara mijini na vijijini (TARURA) Arcad Tesha amesema mbali mradi huo pia kuna barabara ya njia panda ya Soweto hadi Sanje ina urefu wa kilomita 8 inatarajiwa  kumwaga kifusi kwenye eneo la kilomita tatu za barabara hiyo.

Sambamba na kuongeza nguvu ujenzi wa daraja linalounganisha vijiji vya Sanje na Itizi kutokana na daraja hilo kutopitika hali ambayo itachochea shughuli za kiuchumi.

Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza amesisitiza wataalam wa barabara mjini na vijijini (TARURA) kutimiza matakwa ya mikataba ili wananchi wasogezewe huduma muhimu husasani za barabara na maji.

Kwa upande wake Ofisa mipango Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Beatrice Keffa Urio, amesema wako  kuwatumikia wananchi wataendelea kutekeleza miradi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment