Tuesday, July 9, 2024

DC: MALISA ATAKA WATU WENYE UALBINO WALINDWE


Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa ameagiza viongozi wa serikali za mitaa kuchukua hatua ya kuelimisha jamii kuwalinda watu wenye ualbino.

Malisa amesema leo Jumatatu Julai 8, 2024 kwenye maadhimisho ya siku ya afya ya ngozi duniani iliyofanyika kitaifa Mkoa wa Mbeya na kuratibiwa na Shirika la Standing Voice kwa kushirikiana na Hosptali ya Rufaa ya Mkoa.

Amesema sasa imefika mwisho kwa watu ambao wanatafuta mali kwa kuwaua albino na kisha kwenda kuuza viungo vyao watakao bainika sheria itachukua mkondo wake.

"Hivi karibuni Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa viongozi wa serikali hususan sisi wakuu wa Wilaya  kuona albino wanalindwa  kuwa salama nimetoa maelekezo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa kubeba suala hilo kama ajenda kwa lengo la kuhakikisha wako salama na kukemea vitendo hivyo" amesema Malisa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Godson Mollel amesema matukio ya mauaji yanayo fanyika yanalichafua taifa la Tanzania na kuwaweka kwenye kipindi cha hali ya hofu kubwa.

"Tunaomba hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika kunyongwa hadi kufa kwani sasa wamechoka wanaishi kwa hofu na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi kula na kulala vizuri kutokana na watu wachache kuwawinda.

Meneja uendeshaji wa shirika la standing voice, Alex Maganga amesema mbali na kuadhimisha siku ya afya ya ngozi watatoa elimu ya kukabiliana na magonjwa ya saratani.

Amesema kuanzia leo Julai 8 watatoa huduma ya vipimo na matibabu bure kwa watu wenye ualbino kwa kipindi cha siku 10 na kutoa vifaa vya kujikinga na mionzi ya jua

Dkt. Harry amesema programu hiyo itawanufaisha watu 9,000 nchini huku mikoa ya Mbeya na Iringa itakuwa miongoni lengo ni kuona kundi hilo linakuwa salama katika kukabiliana naa saratani ya ngozi.

No comments:

Post a Comment