Menejimenti ya hospitali, wakiwemo watendaji kutoka Idara mbalimbali za Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) leo Julai 11, 2024 wamepewa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Government Assets Management Information System (GAMIS) ili kuwawezesha kuingiza na kuhuisha taarifa za mali za taasisi kwenye mfumo kwa wakati.
Mafunzo hayo yametolewa na wakufunzi kutoka Wizara ya Fedha Said Mtatura na Simon Njoka ambaye pia ni msimamizi wa mali za Serikali Mkoa wa Mbeya na Songwe na kueleza kuwa mafunzo hayo ni wezeshi kwa maafisa usimamizi wa mali za Serikali hususani maafisa wapya kwa lengo la kuwajengea uwezo kwenye matumizi ya moduli zilizopo kwenye Mfumo wa GAMIS.
Akihitimisha mafunzo hayo ya siku 4 kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Mkurugenzi wa Utawala na Huduma Shirikishi Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Myriam Msalale ameishukuru wizara ya fedha na wakufunzi kwa kuwajengea uwezo watumishi wa Hospitali hiyo ili waweze kutumia mfumo kwa usahihi.
Msalale amewapongeza watumishi walioshiriki katika mafunzo hayo na kutaka kuwa waalimu kwa wengine kwenye programu GAMIS kwa matokeo ya usalama, faida na matumizi kwa hospitali.
"Tumeaona faida nyingi katika mafunzo haya, matumizi sahihi ya mfumo wa GAMIS hususani moduli mama ya usajili wa mali na moduli nyingine zilizopo katika mfumo huo yanatuwezesha kutambua kiasi, idadi, hali na mali zilizopo na kuziwezesha taasisi kufunga hesabu za fedha kwa kutumia taarifa zilizopo katika Mfumo wa GAMIS kama ilivyoelekezwa kupitia waraka wa Hazina Na. 2 wa mwaka 2021/2022” amesema Msalale.
Katika jitihada za kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na kuendana na uchumi wa kidigitali, Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mali za Serikali (GAMIS) kwa lengo la kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mali za umma pamoja na kuondoa changamoto zilizopo.
No comments:
Post a Comment