Friday, July 12, 2024

MGANGA WA KIENYEJI MATATANI KWA KUZINI NA MAHARIM

Masumbuko Wenson Sompo (51) Mkazi wa Sangambi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya amefikishwa Mahakama ya Wilaya kwa tuhuma za kuzini na maharim.

Akisoma hati ya mashitaka kesi ya jinai namba 19278/ 2024 Kaihwa Stephen Mayanja mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Chunya James Mhanusi amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo juni 23, 2024 porini majira ya saa tisa usiku.

Mayanja amesema kosa hilo ni kinyume cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kifungu cha 158 (1) (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ambapo mshitakiwa amekana kutenda kosa.

Mwendesha mashitaka amesema upelelezi umekamilika na upande wake utakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili.

Shahidi wa kwanza ambaye ni mtendewa akiongozwa na Mwendesha Mashitaka amesema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari mwenye umri wa miaka kumi na saba na kwamba mtuhumiwa aliyepo mbele ya Mahakama ni baba yake mzazi ambaye alimbaka saa tisa usiku na kwamba angepiga kelele angemuua hivyo alishindwa kupiga kelele kwa hofu ya kuuawa.

Hata hivyo muda mfupi baada ya kutendewa ukatili huo alisikia sauti ya Zawadi Minga ambaye ni mama yake mdogo, Lucia na kaka yake aitwaye Baraka Sompo ambao walisikika wakiita jina la baba yake.

Aidha binti ameiambia Mahakama kuwa watu hao walimwamuru kuondoka eneo hilo ndipo alidai majira ya saa tatu usiku akiwa porini alikutwa na mama mmoja ambaye alimchukua na kwenda nyumbani kwake kisha kumpigia simu mama yake mdogo aliyepo Mbeya ambaye alimuomba mama huyo amhifadhi kwake ndipo alimtumia nauli hadi Mbeya na baadaye Mbozi kwa mjomba wake ambaye alishauri watoe taarifa Ofisi za haki za binadamu Mbeya.

Ofisi za haki za binadamu baada ya kulipokea shauri hilo waliagiza taarifa lipelekwe Polisi Chunya ambao walimwandikia barua Ustawi wa Jamii Chunya ambao waliamuru atibiwe. Baada ya matibabu ndipo alipokuja mahakamani, alisema shahidi.

Mtuhumiwa alipopata muda wa kuuliza maswali baada ya ruksa ya Hakimu James Mhanusi Masumbuko Wenson Sompo aliniuliza binti yake alibakwa muda gani binti alijibu alibakwa na baba yake saa tisa usiku.

Swali jingine mtuhumiwa aliulizwa mazingira yalikuwaje binti alijibu porini karibu na nyumbani,pia mtuhumiwa aliuliza alijuaje kuwa ni saa tisa usiku binti alijibu kuwa aliwasikia watu waliokuwa wakizungumza karibu na eneo la tukio.

Mtuhumiwa hakuwa na maswali mengine ambapo Hakimu James Mhanusi amesema dhamana ya maandishi iko wazi kwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa Mtendaji na mali zisizohamishika zenye thamani ya shilingi milioni nne kila mmoja na kipindi cha kesi hapaswi kusafiri kwa mujibu wa kifungu namba 148 sura ya 6 (b) sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mhanusi ameahirisha kesi hadi Julai 24, 2024 upande wa mashitaka utakapoleta mashahidi wengine na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu kutokana na kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.

No comments:

Post a Comment