Thursday, July 11, 2024

RUNGWE KUTUMIA NGOMA ZA ASILI KUTANGAZA UTALII

Mbunge wa Jimbo la Rungwe, Athon Mwantona ameanzisha mashindano ya ngoma za asili,nyimbo za injili na mashindano ya mpira wa miguu kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji kwenye utalii.

 Katibu wa Mbunge, Gabriel Mwakagenda amesema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mipango mikakati ya kuitangaza Wilaya ya Rungwe na kuvutia uwekezaji.

Mwakagenda amesema Wilaya ya Rungwe ina vivutio vingi vya utalii ambavyo vikitumika vinatengeneza fursa za kiuchumi kwa vijana na hata mapato kwa serikali.


"Mikakati ya Mbunge kuhamasisha katika masuala mbalimbali kama michezo ya mpira wa miguu,pete na ngoma za asili na kwaya za madhehebu ya kidini kutunga nyimbo zenye kutangaza fursa za uwekezaji" amesema.

Amesema  pia Mbunge Mwantona atafanya ziara ya katika Kata 12 zenye vijiji 43 kueleza mambo ambayo serikali ya awamu ya sita imetekeleza chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Sambamba na hilo Mwakagenda amesema kuwa wamendaa ligi kuanzia ngazi ya kata, kanda na Jimbo lengo ni kuhamasisha michezo, kuibua vipaji na kupata timu itakayoshiriki ligi ngazi ya Mkoa na ligi kuu.

No comments:

Post a Comment