Wednesday, February 14, 2024

POLISI WATAKIWA KUTUNZA MITI KWA FAIDA YA KIZAZI KIJACHO.

 
Polisi Mkoani Mbeya wametakiwa kupanda miti, kuilinda na kuitunza miti hiyo iliyopandwa katika maeneo yao kwa faida ya kizazi kijacho.
 
Wito huo umetolewa leo Februari 14, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwa Polisi Mkoa wa Mbeya lililofanyika katika uwanja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani hapa.

Kuzaga amesema kuwa, zoezi la upandaji miti katika maeneo ya kambi za Polisi, vituo vya Polisi na maeneo mengine ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura.

Ameongeza kuwa zoezi hilo litafanyika katika Wilaya zote sita za Kipolisi za Mkoa wa Mbeya ambapo kila askari amekabidhiwa mche wa mti kwa ajili ya kupanda na kuhakikisha anautunza ili kufikia malengo ya Jeshi na nchi kwa ujumla.

Pia Kuzaga amesema kuwa, zoezi lililofanyika leo, jumla ya miche ya miti ya matunda na kivuli elfu moja aina ya Kassuarina, Pinuspatula, Misongwa na Mizambarao imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment