Friday, February 9, 2024

DC MALISA AWAKUMBUSHA MSD KUSIMAMIA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA KUKUSANYA MAPATO.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa imeitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Nyanda za Juu Kusini  kuvisimamia vituo vya kutoa huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya ikiwepo ununuzi wa bidhaa.

Malisa amesema leo Ijumaa Februari 9, 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau wa afya na watoa huduma mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Juma Homera.

Amesema Bohari ya Dawa Kanda ya Mbeya inatekeleza majukumu mawili ya kutunza na kusambaza bidhaa kwenye halmashauri 17 zenye vituo vya afya vya kutolea huduma za ya 884 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Makete Mkoa wa Njombe.


Amesema ili kuboresha utoaji huduma za afya kila mmoja analo jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya ili kuleta tija kwa wananchi na kupunguza manung'uniko.

“Kupitia mkutano huu natumaini wadau wa MSD kupitia Wizara ya afya, kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi na wakati ili kusaidia kuwa na takwimu sahihi wa kuweza kuboresha huduma bora kwa watanzania” amesema.

Wakati huo huo ameagiza waganga wakuu wa mikoa ,wilaya na wafamasia kukagua na kufuatilia matumizi bora ya bidhaa za afya katika kila ngazi ili kudhibiti mianya ya upotevu mapato.

Upande wake Meneja wa MSD Kanda ya Nyanda za Juu Marco Masala amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kupata fursa ya kujadiliana na kutatua changamoto za upatikanaji wa bidhaa za afya katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Amesema kuwa kwa kila mmoja atatoa mawazo yake kwa uwazi na Uhuru ili kuweza kutoka na matokeo mazuri ambayo yatakuwa mwarobaini wa kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa vifaa tiba.

Wakati huo huo amesema wameweza kutoa tuzo kwa baadhi ya halmashauri ambazo zimefanya vizuri katika malipo ya madeni, uagizaji wa bidhaa za afya kwa wakati pasipo kutegemea mapato kutoka serikalini.

Miongoni mwa Halmashauri zilizopata tuzo ni pamoja na Mbeya Jiji, Mbeya Dc, Tunduma, Kyela, Chunya, Rungwe na Busokelo.

No comments:

Post a Comment