Monday, February 19, 2024

POWERTILLAR, PIKIPIKI ZATUMIKA KUWAFIKIA WANANCHI KUTOA CHANJO, MBARALI

 


Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwela akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mara baada ya uzinduzi wa chanjo ya Surua na Rubella.


Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya imelazimika kutumia usafiri wa bodaboda na Powertiller kwa ajili ya kuwafikisha wataalam wa afya kwa ajili ya kutoa chanjo ya surua na rubella katika maeneo yasiyofikika.

Hatua hiyo ilitokana na  na changamoto ya baadhi ya maeneo kupata athari za uharibifu wa miundombinu ikiwepo kukatika kwa mawasiliano ya barabara, vivuko, madaraja na makaravati kuharibiwa na maji ya mvua yaliyosababisha mafuriko  Januari 30 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Missana Kwangura akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mkurugenzi wa halmashauri, Missana Kwangura amewaambia waandishi habari kwamba matarajio ni  kutoa chanjo kwa watoto 64,343 huku wakiwa wamepokea chanjo 74,000 ikiwepo ziada ya 5,000.

“Zoezi la chanjo tumezindua jana rasmi na tayari watalaam zaidi ya 200 wamesambazwa kwenye vituo 80 tulivyopanga ingawa kuna changamoto ya namna ya kufika maeneo ambayo mawasiliano yamekatika ambako watalazimika kutumia usafiri bodaboda na powertiller ”amesema.

Kwangura amesema  tayari wametoa maelekezo kwa wataalam kwenye maeneo ambayo magari hayafiki watumie usafiri huo lengo ni kufikia matarajio ya kuchanja idadi hiyo ya watoto licha ya kuwepo na vipindi vigumu kwani kuna maeneo maji ni mengi.

Kwangura pia  wamelazimika kutumia wenyeviti wa Serikali za vijiji na mitaa kuhakikisha watoto wote walio na miezi tisa mpaka miaka mitano wanapata chanjo ya surua na rubella na kuwasaka wazazi ambao watawaficha wakiwepo jamii ya wakulima na wafugaji.

“Lengo la kuwatumia wenyeviti wao ndio wenye watu na wanajua idadi iliyopo kwenye maeneo yao hivyo wanauhakika watafikia kuchanja watoto 69,343 na kutumia chanjo yote dozi 74,000” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (DC) Kanali Denis Mwela amesema tayari Serikali imetoa Sh 80 milioni kwa ajili ya malipo ya wataalam wa afya 200 waliosambazwa kwenye vituo vilivyoelekezwa.

Mwela amesema kuwa matarajio yao watoto wote na ambao hawajapata chanjo wanapatiwa kwa utaratibu maalum iwe mvua liwe jua sambamba na kuwataka wenyeviti wa vijiji ,mitaa na vitongoji kutoa ushirikiano kwa wataalam nyumba kwa nyumba.

“Pia tumeshirikisha viongozi wa mira,dini kuona ni jukumu lao kuisadia Serikali kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto kupata chanjo lengo ni kuwakinga watoto na magonjwa katika ukuaji” amesema.

Kwa upande wake Neema  Shija  wa jamii ya wafugaji,amesema kwa miaka ya sasa wamepata elimu ya kujua umuhimu wa chanjo kwa watoto na kueleza wako tayari kutoa ushirikiano kwa kuwapeleka watoto.

“Miaka ya nyuma tulikuwa tunawaficha watoto tunapoona matangazo ya chanjo ya wataalam wanapopita nyumba kwa nyumba kwa kuamini ina madhara ikiwepo ulemavu wa kudumu kwa watoto” amesema.

No comments:

Post a Comment