Na Joachim Nyambo, Mbeya.
SURUA ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya “Morbillivirus paramyxovirus” vinavyoenea kwa haraka kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hasa sehemu zenye msongamano. Unaenezwa kwa njia ya hewa pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya.Ugonjwa huu huathiri watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi.
Kwa hapa nchini tangu mwaka 1975 Wizara ya Afya imekuwa ikitoa dozi moja ya Chanjo dhidi ya surua kwa mtoto anapofikisha umri wa miezi tisa na pia wakati wa kampeni. Lakini kuanzia mwaka 2014, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeongeza dozi ya pili ya surua kwa mtoto anapofikisha umri wa miezi kumi na nane.
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na Homa na vipele vidogo vidogo hutokea ambavyo huanza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima. Dalili nyingine ni Macho kuwa mekundu, Mafua na kikohozi. Hivyo wataalamu wa Afya wanashauri mtu anapoona mojawapo ya dalili hizi ampeleke mtoto kwenye kituo cha huduma za afya haraka kwa uchunguzi, matibabu na ushauri.
Madhara ya ugonjwa wa surua ni pamoja Kuhara kunakoweza kusababisha upungufu wa maji na chumvi chumvi mwilini, Nimonia, Masikio kutoa usaha ambao huweza kusababisha mtu kuwa kiziwi, Vidonda vya macho vinavyoweza kusababisha upofu, Utapiamlo na pia Kifo huweza kutokea.
Kwakuwa ugonjwa huu hauna tiba wataalamu wanashauri kuzingatia utolewaji wa chanjo kwa namna utaratibu livyowekwa Mamlaka husika kwakuwa unaweza kuzuilika. Yaani Chanjo ya kwanza mtoto anapaswa miezi tisa ambapo hutolewa sambamba na matoneya vitamini A na chanjo ya pili mtoto anapotimiza umwri wa miezi kumi na nane sawa na mwaka mmoja na nusu. Sambamba na chanjo hizo mbili mtoto pia anatakiwa kupata chanjo ya surua zinapotokea kampeni za chanjo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, utoaji wa chanjo zote mbili za surua kwa watoto kulingana na ratiba kunawapa kinga kamili. Manufaa mengine ni kupunguza maradhi na madhara ya surua, kupunguza vifo vitokanavyo na surua, kupunguza gharama ya kuuguza wagonjwa wa surua, kutokomeza ugonjwa wa surua.
Kama ilivyo utaratibu wa wizara hivi sasa nchini inaendelea Kampeni yay a Utoaji Chanjo ya Surua na Rubella ikifanyika nchi nzima. Imeanza kutekelezwa leo Februali15 na itamalizika Februali 18 katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na maeneo maalumu yaliyoandaliwa.
Kwa mkoani Mbeya kupitia Kampeni hii watoto 348,604 wenye umri wa miezi tisa hadi miaka mitano,wanatarajia kupata Chanjo ya sindano ya kupambana na ugonjwa wa Surua na Rubella. Inahusisha umri huo kwakuwa ni kampeni maalumu na si utaratibu wa zile awamu mbili za chanjo.
Kupitia Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alitoa onyo kwa wapotoshaji wa zoezi la chanjo ya Surua Rubella kuwa watachukuliwa hatua za kisheria kwani kufanya hivyo ni kuhujumu afya za watoto wa Mkoa wa Mbeya.
Homera anasema lengo la Serikali kutoa chanjo hiyo ni kuimarisha kinga kwa watoto ili wasipatwe na ugonjwa huo na hivyo akawaomba viongozi katika maeneo mbalimbali pamoja na wananchi kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha lengo la kampeni hiyo linatimia.
Kampeni hii ilifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 15 - 18 Februari katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na maeneo maalum yaliyoandaliwa.
“Lengo kuu la kampeni ni kuzuia kuenea kwa ugonjwa Surua na Rubella na kuongeza kinga kwa walengwa hata kama wameshapata chanjo katika utaratibu wa kawaida wa kutoa huduma za chanjo.”
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mbeya, Dkt. Danford Barnabas alinasema aina ya chanjo zinazotolewa ni zile zile za siku zote na kwamba wanalenga pia kuwapata watoto ambao kwa sababu mbalimbali hawakupata chanjo za awali ili kuhakikisha kila mtoto anayestahili kupata chanjo anapatiwa.
Dkt. Barnabas anasema utoaji wa chanjo unahusisha,vituo vya kudumu vya kutolea huduma za afya,kliniki tembezi na vituo vilivyoundwa na kuhusisha maeneo mbalimbali ikiwemo, masoko, shule, nyumba za ibada, mashambani, vituo vya mabasi kambi za wakimbizi, vituo vya mipakani na sehemu zote ambazo watoto wanapatikana.
Dkt. Elizabeth Nyema ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya , anasema Mkoa umepokea dozi 398,000 kwa ajili ya utoaji chanjo kampeni hiyo na kuongeza kuwa mkoa unao wataalamu wa kutosha kwa ajili ya zoezi hilo.
Anasema timu ya wataalamu zaidi ya 400 wakiwemo wataalamu wa afya na wale waliopewa mafunzo watapita katika maeneo yote yenye watoto kwa ajili ya utoaji chanjo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk. Boniface Makeremo, aliomba wataalamu kuangazia zaidi maeneo ya pembezoni ambayo hayafikiki kwa urahisi hususani pembezoni mwa miji ili kuwafikia watoto wote.
Muhimu kwa jamii ni kutambua kuwa gonjwa wa Surua hauna tiba, bali matibabu hutolewa kwa ajili ya kutibu madhara yaliyosababishwa na surua kama vile homa, kuhara, nimonia au masikio yenye kutoa usaha. Mtoto mwenye surua apewe vinywaji na chakula cha kutosha.
Ni wakati kwa wazazi na walezi wa watoto walio na umri unaotajwa wakatoa ushirikiano kwa wataalamu kwa kuwapeleka watoto wao kwenye vituo husika ili wapate chanjo hii. Hii itaepusha madhara kwa watoto na kuoepusha athari kwa familia, jamii wanamoishi na Taifa kwa ujumla.
Hakikisha mtoto wako anakamilisha chanjo zote mbili dhidi ya surua kulingana na ratiba kwa kinga kamili. Chanjo zote zinatolewa bila malipo katika vituo vyote vya huduma za afya.
No comments:
Post a Comment