Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa amewataka Madiwani kuanza ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu wa kodi za watanzania.
Issa amesema Leo Jumanne, Februari 13, 2024 wakati akifunga kikao cha baraza la madiwani cha kawaida cha kupendekeza bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ya zaidi ya Sh 91 bilioni.
Issa amesema umefika wakati madiwani katika maeneo yao kuisadia Serikali kufuatia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi hatua kwa hatua sambamba na kutoa taarifa kwa ambayo wataitilia mashaka.
“Madiwani Serikali inashusha fedha nyingi sana za miradi kwenye kata zenu sasa fuatilieni hatua kwa hatua kubaini uhalisia wa matumizi kwani tumepata fedha nyingi za miradi, sambamba na kumshukuru Mbunge, Dkt. Tulia Ackson kwani amekuwa kiungo kikubwa kwa hatua za maendeleo tuliyopiga kama Jiji” amesema.
Katika hatua nyingine, Issa amesema kuwa mpaka sasa halmashauri inaendelea na ukamilishaji wa maboma ya vyumba 54 vya madarasa kwenye miradi ambayo imejengwa na wananchi.
Issa amesema Halmashauri imeanza utaratibu wa kuboresha miundombinu ya Shule za msingi na Sekondari kongwe jijini hapa huku Shule huku ya Isyenye Kata ya Ilomba ikitengewa zaidi ya Sh 150 milioni
Mkurugenzi wa Halmashauri, John Nchimbi amesema kuwa kwa sasa Jiji linatumia makachero kufuatilia upotevu wa fedha unaofanywa na watu wachache katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani.
“Tumepata taarifa na tumeanza ufuatiliaji wapo ambayo tumewabaini na tuna video ambazo zimerekodiwa kabisa na watu maalum tutaleta kwenu baada ya utaratibu zote kukamilika kwani wamekuwa wakiweka fedha mifukoni badala ya kuingiza kwenye mifumo ya kielekriniki na kusabisha upotevu wa mapato ya ndani” amesema.
Aidha katika hatua nyingine Nchimbi amesema kuwa zaidi ya Sh 900 milioni zimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya vijana kwa ajili ya ununuzi wa magari mawili ya kuzoelea taka ikiwa ni sehemu ya kujikwanua kiuchumi.
Naye Diwani Kata ya Sisimba, Josephine Kamunga ameomba halmashauri ya Jiji kuharakisha kuweka mradi kwenye eneo la soko kuu la uhindini lililiteketea kwa moto mwaka 2010 ili kuepuka kutumika kwa matumizi yasiyo sahihi na wananchi.
“Mkurugenzi eneo la wazi lililokuwa soko kuu la uwindini lipo wazi kwa miaka zaidi ya 15 tunaomba liangaliwe ili kuweze kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya ndani ya halmashauri yetu”.
No comments:
Post a Comment