Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda ameagiza wananchi wa Kijiji cha Ndanga Kata ya Mbuyuni ambao nyumba zao zimeathiriwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha waondoke katika eneo huku akiutaka uongozi wa Kata hiyo kufanya tathimini na kusimamia zoezi la wananchi hao kuhama.
Itunda ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea eneo hilo ambapo, zaidi ya kaya 100 zimaathirika baada ya maji kujaa kwenye makazi yao na kuharibu nyumba na vitu mbalimbali.
“Maeneo ambayo yamekumbwa na changamoto hii katika Wilaya yetu ni mengi. Maeneo mengine ya miundombinu ya barabara imekumbwa na changamoto ya mafuriko, tumepita na meneja wa TANROADS mkoa kuhakikisha kwamba barabara zote ziapitia” ameeleza DC Itunda ambaye alilazimika kupanda bodaboda kilomita zaidi ya tano ili kufika katika eneo hilo baada ya gari kushindwa kupita.
“Naomba niwape pole sana ndugu zangu, nimejionea mwenyewe adha na changamoto mnayokumbana nayo. Nimewaona mama zangu wengine wamebeba watoto wengine wamebeba mizigo wanavyopita kwenye eneo hili kama wanaogelea kwa sababu njia zote zimejaa maji.
“Tumetembea juu ya maji na sikuona sehemu ambayo iko salama, niwapongeze bodaboda wakati mwingine nilikuwa nahofu kuwa atanidondosha. Baada ya kujionea na kuwasikiliza naungana na viongozi wenu kuwa wale walioshauri kuondoka kwenye eneo hili naagiza kuanzia sasa waondoke kwenye makazi yao” amesisitiza DC Itunda ambaye aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe, Ndugu Reuben Chongolo, Afisa Tarafa ya Kwimba na Diwani wa Kata ya Mbuyuni.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua zinazoendea kunyesha katika Wilaya ya Songwe kuanzia Januari 30, 2024 ambapo maeneo mengi katika Kata ya Mbuyuni na Magamba yamejaa maji.
No comments:
Post a Comment