Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe Solomon Itunda amesimamisha mchakato wa utoaji leseni ulioanza kutolewa eneo la Bafex lililopo mlima Elizabeth Kata ya Saza Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.
Itunda amechukua hatua hiyo katika mkutano wa wachimbaji wadogo wadogo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Songwe Philip Mulugo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe Abraham Sambila na kamati ya usalama ya Wilaya ya Songwe.
Awali Itunda amepokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa wachimbaji Shadrack Mwakyalabwe, Benedict Mwakitonga na Michael Matoke ambao kwa pamoja wao kupitia kikundi cha Songwe Gold Family wameomba leseni thelathini na nne lakini badala yake wakaambiwa kuwa leseni zinazopaswa kulipiwa ni mbuli tu hali iliyozua taharuki kwa wachimbaji ambao walilazimika kufika ofisi ya Madini ili kupata ukweli wa jambo hilo.
Viongozi hao ambao walikuwa na mchakato na Mkuu wa Wilaya ili kuona namna ya kuumaliza mgogoro huo baada ya kampuni ya Bafex kushinda kesi na mlima huo kurejeshwa serikalini.
Wakati Mkuu wa Wilaya akiendelea kufanya mazungumzo alishangazwa na taarifa za kuwepo kwa leseni zilizolipiwa na UWT pia Jumuia ya Wazazi kinyume na makubalino ya awali kuwa wachimbaji wajiorodheshe ili wafanyiwe maombi ya kulipiwa leseni thelathini na nne.
Aidha katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ameagiza wachimbaji waendelee na shughuli zao mpaka watakapopata taarifa nyingine.
Hata hivyo ameunda tume kwenda kumuona Mkuu wa Mkoa Songwe sanjari na Waziri wa nishati na Madini ili kupata suluhu ya mgogoro huo ambao umezua hofu ya wachimbaji kunyang'anywa maeneo yao.
"Nipo hapa kumuwakilisha Rais hivyo sitapenda wananchi wapate karaha ya aina yoyote na kuhakikisha nazilinda kura za Rais"alisema Itunda
Kwa upande wake Mbunge wa Songwe Philip Mulugo amesema katu hawezi kuwasaliti wananchi wake kwani tangu muda mrefu amekuwa akilipigania eneo hilo kwani limekuwa likichangia pato la Wilaya,Mkoa na Taifa.
"Nilimuomba Mheshimiwa Rais kipindi cha kampeni ya uchaguzi mwaka 2020 kipindi hicho akiwa makamu wa Rais hivyo baada ya serikali kulirejesha mikononi mwake hakukuwa na maombi yoyote na wananchi walikuwa wakiendelea na shughuli zao"alisema Mulugo huku akishangiliwa na wachimbaji.
Mulugo ameahidi kushirikiana na tume iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ili kuhakukisha suala hilo linamalizika kwa amani.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe amesema yupo bega kwa bega na wananchi wake ili haki iweze kupatikana.
Fatuma Mussa ni mmoja wa wachimbaji amesema wao kama wachimbaji wameajiri vijana wengi hivyo kunywang'anywa maeneo yao kutaleta athari kubwa kwenye jamii hivyo ameiomba serikali kulichukua jambo hilo kwa uzito mkubwa.
Tume hiyo iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya itakwenda Dodoma ili wachimbaji kupitia kikundi chao waweze kupatiwa leseni zao.
No comments:
Post a Comment