Friday, February 16, 2024

MAKALA: WANAONYONYESHA WANATAKIWA KUWA KARIBU NA WENZA KUEPUKA KUKOSA MAZIWA.

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila (katikati) akitoa elimu ya umuhimu ya makundi mbalimbali ya vyakula kwaajili ya lishe ya mtoto kwenye kongamano la kuhitimisha Mafunzo ya Malezi na Makuzi kupitia mtandao yaliyoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation yaliyobeba kaulimbiu ya Elimika sasa kwa njia ya Mtandao yakiwalenga akinamama wajawazito na walio na watoto wachanga. (Picha na Joachim Nyambo).

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila akitoa elimu ya umuhimu ya makundi mbalimbali ya vyakula kwaajili ya lishe ya mtoto kwenye kongamano la kuhitimisha Mafunzo ya Malezi na Makuzi kupitia mtandao yaliyoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation yaliyobeba kaulimbiu ya Elimika sasa kwa njia ya Mtandao yakiwalenga akinamama wajawazito na walio na watoto wachanga. (Picha na Joachim Nyambo).
 

Wanawake wanaonyonyesha kukosa ushirikiano wa karibu kutoka kwa wenza wao imetajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuwaletea msongo wa mawazo wenye kusababisha kukosa maziwa mengi ya kunyonyesha watoto wao.

Inaelezwa kuwa hakuna mama aliye na maziwa machache bali zipo sababu nyingi ambazo hupelekea changamoto hiyo na miongoni mwa hizo ni pamoja na mama anayenyonyesha kuwa na msongo wa mawazo.

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila alibainisha hayo kwenye kongamano la kuhitimisha Mafunzo ya Malezi na Makuzi kupitia mtandao yaliyoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation yaliyobeba kaulimbiu ya Elimika sasa kwa njia ya Mtandao yakizilenga familia za akinamama wajawazito na walio na watoto wachanga.

Katika Kongamano hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kitengo cha Wazazi Meta, Mlagila alitaka jamii kuondokana na dhana potofu ya kuwepo kwa mama wanaonyonyesha wasiotoa maziwa mengi na badala yake zitazamwe sababu zinazomsababishia mwanamke husika changamoto hiyo ili kupata ufumbuzi.

Alisema ufumbuzi moja wapo kwenye kupambana na mama kukosa maziwa ya kutosha ni pamoja na mwenza wake kuwa karibu naye katika kipindi cha unyonyeshaji badala ya kumkimbia au kumfanyia unyanyasaji kama inavyoonekana kwenye baadhi ya familia.

“Wengi wetu tumezoea kulalamika ooh mimi sina maziwa mengi!..hapana hakuna mama aliye na maziwa mepesi wala machache. Zipo sababu zinazoleta hali hiyo na miongoni mwa hizo ni mama kuwa na stress…usiwe na stress(msongo wa mawazo). Na sababu zinazopelekea stress ni pamoja na kuwa mbali na mwenza.” Alisema Mlagila

Afisa huyo aliitaja sababu nyingine ya mama kutotoa maziwa mengi au mepesi kuwa ni kutonyonyesha mara kwa mara hatua inavyosababisha vichocheo vya mwili kutosisimuliwa akisema kadiri unyonyeshaji unavyofanyika ndipo mwili hujipanga kuzalisha maziwa kwa kiwango kikubwa zaidi.

Kwa upande wake  Mratibu msaidizi wa Chanjo katika Kitengo cha wazazi Meta, Zena Sambala alisisitiza suala la mama wajawazito na wanaonyonyesha kufika na wenza wao wanapohudhuria kliniki au matibau mengine kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya ili kupata uelewa wa pamoja wa mambo muhimu yanayohitajika kufanyika.

Sambala pia alisisitiza watoto wanaopata changamoto baada ya kupewa chanjo kurejeshwa kwenye vituo walivyopewa huduma iliafanyiwe uchunguzi akisema hiyo itawezesha pia wataalamu kujua chanjo husika imeonekana kuwa na madhara kwa kiwango gani.

Marium Hamis ni miongoni mwa wanawake walionufaika na elimu hiyo kupitia mtandao tangu angali mjamzito mpaka anajifungua ambaye alisema kupitia group sogozi la WhatsApp yeye na wenzie walipata fursa kubwa ya kujifunza masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (MMMAM).

Mkurugenzi Mtendaji wa WeCare Foundation, Elizabeth Maginga alisema waliamua kuanzisha mafunzo ya MMMAM kupitia mtandao ili kuwafikia kwa urahisi wahitaji huku siku ya kilele wakiyapa nguvu maeneo ambayo washiriki hawakuyaelewa kwwa kina kwenye kundi ambayo ni pamoja na lishe toshelezi, malezi ya uchangamsi na chanjo.

Alisema katika mafunzo hayo yaliyoanza Agosti mwaka jana zadidi ya akina mama 250 waliojiunga na kundi sogozi walipata elimu huku akisema maafunzo kama hayo tena yataanza mwezi ujao.

 

No comments:

Post a Comment