Tuesday, February 27, 2024

CCM YATOA MWELEKEO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KUTOWABEBA WAGOMBEA


Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa ( NEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza msimamo wake kuelekea uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa kutombeba mgombea yoyote na badala yake kuwataka kujipima wenyewe kama watakubalika kwa wananchi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM  Taifa (NEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema Jana  wakati akizungumzia msimamo wa chama kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika hivi karibuni sambamba na kuonya walioanza kupasha kutangaza nia kabla ya wakati.

“Hao walioanza  kupitapita huko wanapoteza muda kwani kuna hatua za awali za michakato kuanzia ngazi za Kata, Mitaa, Wilaya na Mkoa unafanya maamuzi na sio kwamba kila atakayechukua fomu atapitishwa na chama  tunahitaji kupata mgombea anayekubalika na wananchi katika eneo lake” amesema.

Mwaselela ameweka wazi kuwa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa mwaka huu ni mgumu lengo ni kutaka wananchi kupata viongozi watakaokuwa chachu ya kutatua changamoto katika jamii.

“Chama hakitambeba mtu, nasisitiza hakitambeba mtu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa sasa tunahitaji utulivu, mpaka hapo dirisha likifunguliwe wenye sifa watakaostahili na kukubalika na wananchi  wachukue fomu  kwa kuzingatia kanuni na utaratibu ndani ya chama” amesema.

Amesema kama chama wanaamini wananchi ndio watawapima wagombea kwenye mitaa, vijiji, kata, na Wilaya sio chama na kupiga marufuku wanaoanza kupasha kabla ya wakati huku akisisistiza  wasubiri muda ufike .
 
Kwa upande wake Webby Mwambulukutu amesema kwa sasa chama kisitumie nguvu ya kuwabeba na badala yake wananchi wachague viongozi ambao wataendana  na kasi ya Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo.


Mwambulukutu ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho la wafanyabishara wadogo machinga (Shihuma)  amesema kwa umoja wao watafanya vyema kwa kushirikiana na Chama kuhakikisha wanashiriki  katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa na Mkuu Oktoba 2025 .

“Umefika wakati wananchi tupewe nafasi ya kuchagua viongozi tunao wataka kwani watakaomaliza muda  walipita bila kupingwa hawakuwa chaguo la wananchi walio wengi” amesema.

Naye mkazi wa Sae Jenipha Joel ameunga mkono kauli ya uongozi wa chama kutowabeba wagombea ili wakajipime kwa maendeleo waliyopeleka kwenye maeneo yao.

No comments:

Post a Comment