Thursday, February 8, 2024

CHAMA CHA MAPINDUZI KUJA NA MKAKATI MAALUMU WA KULIPENDEZESHA JIJI LA MBEYA.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema atazungumza na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani na Spika wa Bunge ili kuja mkakati wa kuzitengeneza barabara za mitaani, ili kulipendezesha jiji hilo.

Makonda ametoa kauli hiyo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Februari 7, 2024 katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Jijini Mbeya mara baada ya kutoridhishwa na majibu ya Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani humo, Albert Kindole kuhusu ujenzi wa barabara za mitaa ya Jiji hilo.

"Nitafanya mpango wa kuonana na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia, pia tutawasiliana na Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchangerwa) ili kuweka mkakati maalumu wa kulifanya Mbeya liwe jiji kweli kweli," amesema Makonda.

Awali akijibu swali la Makonda kuhusu mikakati ya ujenzi wa barabara, Meneja wa TARURA Kindole amesema barabara nyingi (takribani kilomita 18) za Jiji la Mbeya bajeti yake imeshatoka na wakandarasi wapo kazini, jambo lililoibua kelele za wananchi waliokuwa katika mkutano huo kuashiria bosi huyo haelezi ukweli.

 "Swali langu ni moja umeona hizi kelele zote wewe ukijitathimini unafaa kuwa mtendaji wa kutafuta kura za Rais Samia,” amehoji Makonda.


Katika hatua nyingine Makonda alimuita Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Nyema aeleze Sh700 milioni za vifaa zipo wapi au zimetumikaje, ambapo alijibiwa fedha hizo zimepelekwa katika vituo vya afya.

Makonda akamuuliza kituo cha afya cha Makongorosi kina vifaa tiba? Akajibiwa kuwa wameagiza vifaa tiba, lakini fedha walizopewa bado hazijashuka chini, jambo ambalo mwenezi huyo alishindwa kumuelewa.

"Yaani mmeshapewa, lakini bado hazijashuka, umesema zimepelekwa kwenye vituo swali hawa wana vifaa tiba na wananchi wakienda wanapata huduma?

Dkt. Nyema akijibu,"huduma za wagonjwa wa nje wanapata, lakini huduma za upasuaji hadi vifaatiba na fedha tulipata tangu Septemba mwaka 2023.”

Makonda anaendelea na ziara yake ya mikoa 20 ya Tanzania bara, lengo ikiwa ni kusikiliza kero za wananchi na kupata majibu ya kero hizo kutoka kwa watendaji wa serikali.

No comments:

Post a Comment