Thursday, February 29, 2024

WAKULIMA WA TUMBAKU WATAKA ZOEZI LA UGAWAJI WA PEMBEJEO LISIMAMIWE NA CHUTCU

Mkuu wa Wilaya ya Chunya ,Mbaraka Batenga akizungumza na Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya  Chunya na Songwe katika Mkutano Mkuu wa 24 wa mwaka.

Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa tumbaku Wilaya ya Chunya na Songwe wamekerwa na  Muungano wa Vyama Vikuu vya Ushirika Tanzania (TCJE) kuchelewesha pembejeo za kilimo na kutaka  usambazaji ufanywe na Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku (CHUTCU) ili kunusuru uzalishaji.

Kauli hiyo imetolewa jana February 29, 2024 kwenye Mkutano mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (CHUTCU) ambapo wamedai TCJE kutowafikishia mbolea kwa wakati wakuwa chanzo cha kusababisha mazao yao yasifanye vizuri shambani. 

Meneja Mkuu wa Chama cha kikuu cha wakulima wa Tumbaku (Chutcu)Wilaya ya Chunya Christian Msingwa (kulia)akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya  Mbaraka Batenga.

Mkulima na Mwanachama wa CHUTCU, mawazo mamboleo amesema changamoto ya TCJE kuchelewesha pembejeo zimekuwa zilizoathiri kwenye uzalishaji wa tumbaku na hawakubaliani na TCJE kuendelea kusambaza pembejeo za kilimo badala yake chama kikuu cha ushirika CHUTCU ndio kiwe kinasimamia.

DC HANIU AZINDUA ZOEZI LA CHANJO YA MINYOO NA KICHOCHO

Mkuu wa wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu jana Februari 28, 2024 amezindua zoezi la chanjo ya Minyoo na Kichocho ikiwa ni sehemu ya kutokeza magonjwa yote yasiyopewa kipaumbele katika jamii. Zoezi hilo limefanyika katika shule ya Msingi Katumba Mchanganyiko kata ya Ibighi.

Akizindua zoezi hili Haniu ameagiza wazazi wote kuwapeleka watoto katika maeneo ya kutolea huduma hii ikiwemo Hospitali, zahanati na vituo vya afya sambamba na shule zote za Msingi na Sekondari.

MICHE YA MATUNDA NA KIVULI ZAIDI YA 100 YAPANDWA SHULE YA MPAKANI WILAYANI KYELA


Taasisi ya Living Together Youth Foundation (LTYF) imeendelea na kampeni ya kufungua klabu za mazingira shuleni sanjari na upandaji miti ya matunda na kivuli katika maeneo ya shule, taasisi za umma na binafsi lengo likiwa ni kuhifadhi mazingira pia kujipatia lishe kutokana na matunda pamoja na kujiongezea kipato na kupata vifaa vya ujenzi.

Akizindua klabu ya mazingira na kuendesha zoezi la upandaji miche zaidi ya mia shule ya mchepuo wa kiingereza ya Mpakani, Mkurugenzi wa LTYF Leonatha Likalango amesema watoto wakipewa elimu ya mazingira watakuwa mabalozi wazuri kwani elimu hiyo wataifikisha kwa wazazi wao nyumbani.

Shule hiyo ni mpya na haina miti ya matunda na vivuli hivyo miti hiyo itasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo, upepo, kuwapatia matunda watoto na kuifanya shule iwe na mandhali nzuri na ya kuvutia.

Tuesday, February 27, 2024

CCM YATOA MWELEKEO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KUTOWABEBA WAGOMBEA


Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa ( NEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza msimamo wake kuelekea uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa kutombeba mgombea yoyote na badala yake kuwataka kujipima wenyewe kama watakubalika kwa wananchi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM  Taifa (NEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema Jana  wakati akizungumzia msimamo wa chama kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika hivi karibuni sambamba na kuonya walioanza kupasha kutangaza nia kabla ya wakati.

“Hao walioanza  kupitapita huko wanapoteza muda kwani kuna hatua za awali za michakato kuanzia ngazi za Kata, Mitaa, Wilaya na Mkoa unafanya maamuzi na sio kwamba kila atakayechukua fomu atapitishwa na chama  tunahitaji kupata mgombea anayekubalika na wananchi katika eneo lake” amesema.

Mwaselela ameweka wazi kuwa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa mwaka huu ni mgumu lengo ni kutaka wananchi kupata viongozi watakaokuwa chachu ya kutatua changamoto katika jamii.

“Chama hakitambeba mtu, nasisitiza hakitambeba mtu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa sasa tunahitaji utulivu, mpaka hapo dirisha likifunguliwe wenye sifa watakaostahili na kukubalika na wananchi  wachukue fomu  kwa kuzingatia kanuni na utaratibu ndani ya chama” amesema.

Amesema kama chama wanaamini wananchi ndio watawapima wagombea kwenye mitaa, vijiji, kata, na Wilaya sio chama na kupiga marufuku wanaoanza kupasha kabla ya wakati huku akisisistiza  wasubiri muda ufike .
 
Kwa upande wake Webby Mwambulukutu amesema kwa sasa chama kisitumie nguvu ya kuwabeba na badala yake wananchi wachague viongozi ambao wataendana  na kasi ya Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo.

Saturday, February 24, 2024

WAZEE, WALEMAVU, WENYE MAHITAJI 6,000 WAPEWA BIMA YA AFYA NA DKT. TULIA


Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amefanya tukio la kihistoria katika Mkoa wa Mbeya baada ya kutoa bure kadi za bima kwa kaya 1,000 zenye watu 6,000.

Dkt. Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini ametoa bima hizo ikiwa ni mwendelezo wake wa awamu ya tano ya kusaidia wahitaji kwenye makundi ya walemavu, wazee na wenye mahitaji maalum.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya stendi ya mabasi kabwe , Mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko sambamba na watendaji wa Serikali na Chama.

Akizungumza na maelfu ya wananchi Dkt. Tulia amesema huo ni mpango endelevu wa kutoa bima za afya bure kwa wahitaji na kwamba ni kutokana na uwekezaji mkubwa wa huduma za afya uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

KAMPUNI YA PCT YATOA MSAADA WA MIFUKO 30 YA SARUJI SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI WILAYA YA MBEYA VIJIJINI


Kampuni ya Pareto PCT imetoa msaada wa mifuko 30 ya saruji kwa Shule ya Sekondari Mwakipesile, Shule mbili shikizi katika vijiji vya   Iswago Ruanda.

Kati ya mifuko hiyo 30 mifuko 10 imeelezw kutumika kwa ajili ya  ambayo itatumika kwa  ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na miundombinu ya vyumba vya madarasa.

Msaada huu umetolewa na Kampuni ya PCT kupitia Afisa Pareto wa Mikoa ya Mbeya na Songwe, Mussa Malubalo.

Friday, February 23, 2024

DKT. TULIA AKABIDHI NYUMBA KWA MLEMAVU WA MACHO

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson, amezindua na kumkabidhi nyumba mlemavu wa macho  Hosea Kalemale Mkazi wa Kata ya Mwakibete Jijini.

Makabidhiano hayo yamefanyika Februari 23, 2024  huku mamia ya wananchi wamejitokeza kushuhudia huku wengine wakimuombea Dk Tulia Mungu ampe maisha marefu kwa kitendo cha kijitoa kusaidia wahitaji.
Dkt. Tulia amemkabidhi Hosea nyumba hiyo yenye vyumba viwili vya kulala, sebule pamoja na choo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa siku kadhaa mara baada ya kuombwa hitaji hilo.

“Sitaishia hapa, hata nikifikia hatua ya kuachana na masuala ya kisiasa sitaacha kusaidia watanzania na sio kwamba sasa naacha siasa hapaka ukifika wakati” amefafanua.

Thursday, February 22, 2024

RAIS WA IPU DKT. TULIA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA MBEYA


Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambae pia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, amefika Jimboni kwake na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera.

Mazungumzo hayo yamefanyika  katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa huku pamoja na  mambo mengine wamejadili kuhusu namna bora ya kuboresha Maendeleo ya  Jiji la Mbeya katika sekta mbalimbali.

Wakati huo huo Dkt. Tulia anatarajia kufanya zoezi la kugawa bima za afya bure kwa kaya 600 za jijini hapa.

Lengo ni kuhakikisha jamii inakuwa na afya njema sambamba na kukabidhi nyumba katika Kata ya Mwakibete iliyojengwa kuptia Taasisi yake ya Tulia Trust.

Monday, February 19, 2024

POWERTILLAR, PIKIPIKI ZATUMIKA KUWAFIKIA WANANCHI KUTOA CHANJO, MBARALI

 


Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwela akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mara baada ya uzinduzi wa chanjo ya Surua na Rubella.


Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya imelazimika kutumia usafiri wa bodaboda na Powertiller kwa ajili ya kuwafikisha wataalam wa afya kwa ajili ya kutoa chanjo ya surua na rubella katika maeneo yasiyofikika.

Hatua hiyo ilitokana na  na changamoto ya baadhi ya maeneo kupata athari za uharibifu wa miundombinu ikiwepo kukatika kwa mawasiliano ya barabara, vivuko, madaraja na makaravati kuharibiwa na maji ya mvua yaliyosababisha mafuriko  Januari 30 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Missana Kwangura akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mkurugenzi wa halmashauri, Missana Kwangura amewaambia waandishi habari kwamba matarajio ni  kutoa chanjo kwa watoto 64,343 huku wakiwa wamepokea chanjo 74,000 ikiwepo ziada ya 5,000.

Sunday, February 18, 2024

WAASWA KUCHANGAMKIA KAMPENI YA CHANJO YA SURUA

Na Joachim Nyambo, Mbeya.

SURUA ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya “Morbillivirus paramyxovirus” vinavyoenea kwa haraka kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hasa sehemu zenye msongamano. Unaenezwa kwa njia ya hewa pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya.Ugonjwa huu huathiri watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi.

Kwa hapa nchini tangu mwaka 1975 Wizara ya Afya imekuwa ikitoa dozi moja ya Chanjo dhidi ya surua kwa mtoto anapofikisha umri wa miezi tisa na pia wakati wa kampeni. Lakini kuanzia mwaka 2014, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeongeza dozi ya pili ya surua kwa mtoto anapofikisha umri wa miezi kumi na nane.

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na Homa na vipele vidogo vidogo hutokea ambavyo huanza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima. Dalili nyingine ni Macho kuwa mekundu, Mafua na kikohozi. Hivyo wataalamu wa Afya wanashauri mtu anapoona mojawapo ya dalili hizi ampeleke mtoto kwenye kituo cha huduma za afya haraka kwa uchunguzi, matibabu na ushauri.

Friday, February 16, 2024

MAKALA: WANAONYONYESHA WANATAKIWA KUWA KARIBU NA WENZA KUEPUKA KUKOSA MAZIWA.

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila (katikati) akitoa elimu ya umuhimu ya makundi mbalimbali ya vyakula kwaajili ya lishe ya mtoto kwenye kongamano la kuhitimisha Mafunzo ya Malezi na Makuzi kupitia mtandao yaliyoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation yaliyobeba kaulimbiu ya Elimika sasa kwa njia ya Mtandao yakiwalenga akinamama wajawazito na walio na watoto wachanga. (Picha na Joachim Nyambo).

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila akitoa elimu ya umuhimu ya makundi mbalimbali ya vyakula kwaajili ya lishe ya mtoto kwenye kongamano la kuhitimisha Mafunzo ya Malezi na Makuzi kupitia mtandao yaliyoandaliwa na Shirika la WeCare Foundation yaliyobeba kaulimbiu ya Elimika sasa kwa njia ya Mtandao yakiwalenga akinamama wajawazito na walio na watoto wachanga. (Picha na Joachim Nyambo).
 

Wanawake wanaonyonyesha kukosa ushirikiano wa karibu kutoka kwa wenza wao imetajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuwaletea msongo wa mawazo wenye kusababisha kukosa maziwa mengi ya kunyonyesha watoto wao.

Inaelezwa kuwa hakuna mama aliye na maziwa machache bali zipo sababu nyingi ambazo hupelekea changamoto hiyo na miongoni mwa hizo ni pamoja na mama anayenyonyesha kuwa na msongo wa mawazo.

Thursday, February 15, 2024

TAASISI YA TULIA TRUST YAJA NA MIKAKATI YA KUIHUDUMIA JAMII YA JIJI LA MBEYA 2024.

 Tasisisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Spika wa Bunge, Mbunge wa Mbeya mjini na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) imekuja na mipango kabambe ya kuhudumia jamii ya Jiji la Mbeya huku ikianza kufanya  mazungumzo na  wa Serikali ikiwepo Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na Mstahiki Meya Dormohamed Issa.

Hatua hiyo imeanza kwa mazungumzo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa nyakati tofauti ambapo jana a Februari 13, 2024 wamefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi na Leo Jumatano Februari 14, 2024 wamefika Ofisi ya Mstahiki Meya Dormohamed Issa .

Wakati huo huo wameweza kueleza pia mipango yao kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Malisa kuhusiana na mikakati hiyo Taasisi kuigusa jamii kwa mwaka 2024.

Wednesday, February 14, 2024

JUMATANO YA MAJIVU: TUNAWATAKIA KWARESMA NJEMA.

 

Leo ni Jumatano ya Majivu, siku ambayo ni alama ya kuanza kwa siku 40 za Kwaresma kwa Wakatoliki. Wakatoliki duniani hutumia kipindi hiki kufahamu vizuri kifo na ufufuo wa Yesu kupitia kutubu, kusali, kufunga na kujikana mwenyewe. TUNAWATAKIA MFUNGO MWEMA WA KWARESMA.

DC SONGWE ASIMAMISHA MCHAKATO UTOAJI LESENI MLIMA ELIZABETH.


Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe Solomon Itunda amesimamisha mchakato wa utoaji leseni ulioanza kutolewa eneo la Bafex lililopo mlima Elizabeth Kata ya Saza Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.

Itunda amechukua hatua hiyo katika mkutano wa wachimbaji wadogo wadogo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Songwe Philip Mulugo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe Abraham Sambila na kamati ya usalama ya Wilaya ya Songwe.

Awali Itunda amepokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa wachimbaji Shadrack Mwakyalabwe, Benedict Mwakitonga na Michael Matoke ambao kwa pamoja wao kupitia kikundi cha Songwe Gold Family wameomba leseni thelathini na nne lakini badala yake wakaambiwa kuwa leseni zinazopaswa kulipiwa ni mbuli tu hali iliyozua taharuki kwa wachimbaji ambao walilazimika kufika ofisi ya Madini ili kupata ukweli wa jambo hilo.

POLISI WATAKIWA KUTUNZA MITI KWA FAIDA YA KIZAZI KIJACHO.

 
Polisi Mkoani Mbeya wametakiwa kupanda miti, kuilinda na kuitunza miti hiyo iliyopandwa katika maeneo yao kwa faida ya kizazi kijacho.
 
Wito huo umetolewa leo Februari 14, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwa Polisi Mkoa wa Mbeya lililofanyika katika uwanja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani hapa.

Kuzaga amesema kuwa, zoezi la upandaji miti katika maeneo ya kambi za Polisi, vituo vya Polisi na maeneo mengine ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura.

MRADI LTIP WATATUA MIGOGORO YA MIPAKA SONGWE.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe amesema Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umetatua migogoro ya kimipaka katika halmashauri hiyo hatua inayowasidia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa amani.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Mkwajuni yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo, CPA Kavishe amesema wananchi wa wilaya hiyo ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini, ujio wa mradi wa LTIP umesaidia kutatua migogoro ya mipaka kati ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe na Chunya mkoani Mbeya ambao ulidumu kwa miaka nane tangu kuanzishwa kwa mkoa wa Songwe mwaka 2016.

“Ukiuangalia katika huu mradi hata ulipofika tu siku ya kwanza wakati tunautambulisha kwa wadau, kitu cha kwanza ambacho watu wengi walifurahia kwenye kile kikao ni kwamba tunaenda kutatua migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ya wananchi pamoja na mipaka” amesema CPA Kavishe.

Tuesday, February 13, 2024

'KWA MTOTO ISIISHIE LISHE BORA, LISHE BORA KWA RATIBA SAHIHI'

 

Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo akiwa ameshika kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Uzinduzi wa Programu hiyo katika ngazi ya Halmashauri ya Busokelo iliyopo wilayani Rungwe. (Picha na Joachim Nyambo).

Na Joachim Nyambo.

Wataalamu wa masuala ya Afya wana kauli isemayo ujionavyo ni kutokana na vile unavyokula. Hii ina maana anachokula binadamu au kiumbe hai chochote ndicho huufanya mwili wake uonekane vile ulivyo.

Ni kutokana na hali hiyo wataalamu wa masuala ya lishe wanasisitiza pia umuhimu wa lishe bora kwa watoto kuanzia wakiwa kwenye matumbo ya mama zao, baada ya kuzaliwa na kadiri wanavyoendelea kukua hadi kufikia utu uzima na hadi uzeeni.

 

Afisa Maendeleo ya Jamiii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) baada ya uzinduzi wa Programu hiyo kwenye ngazi ya halmashauri.(Picha na Joachim Nyambo).

Wataalamu wa Afya wanaeleza kuwa Lishe bora kwa mtoto ni sehemu ya mambo muhimu matano yanayowezesha ukuaji stahiki wake. Yaani Lishe inaungana na mambo mengine manne ambayo ni pamoja na Malezi yenye muitikio, Afya bora, Ulinzi na Usalama na Ujifunzaji wa awali.

"MADIWANI TUMIKENI KUDHIBITI UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO" DORMOHAMED ISSA MSTAHIKI MEYA WA JIJI LA MBEYA.


Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa amewataka Madiwani kuanza ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu wa kodi za watanzania.

Issa amesema Leo Jumanne, Februari 13, 2024 wakati akifunga kikao cha baraza la madiwani cha kawaida cha kupendekeza bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ya zaidi ya Sh 91 bilioni.

Issa amesema  umefika wakati madiwani katika maeneo yao kuisadia Serikali kufuatia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi hatua kwa hatua sambamba na  kutoa taarifa kwa ambayo wataitilia mashaka.

“Madiwani Serikali inashusha fedha nyingi sana za miradi kwenye kata zenu sasa fuatilieni hatua kwa hatua kubaini uhalisia wa matumizi kwani tumepata fedha nyingi za miradi, sambamba na kumshukuru Mbunge, Dkt. Tulia Ackson kwani amekuwa kiungo kikubwa kwa hatua za maendeleo tuliyopiga kama Jiji” amesema.

Monday, February 12, 2024

AFISA MTENDAJI WA KATA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA YA LAKI MBILI.

Afisa Mtendaji Kata ya Lusungo, Edestus Clemence Ndunguru amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela kwa shtaka la kuomba na kupokea Rushwa ya Tsh. 200,000 ili amsaidie Mwananchi kuongea na Askari Polisi waweze kumpa dhamana katika Kituo cha Ipinda.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11 ya Mwaka 2007. Mshtakiwa alipelekwa Mahabusu kwa kutokutimiza masharti ya Dhamana huku Kesi ikiahirishwa hadi Februari 20, 2024.

POLISI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UWELEDI NA KUMTANGULIZA MUNGU.

Maafisa wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kumtanguliza Mungu ili kufikia malengo ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi SACP Robert Mkisi amewaasa leo Februari 12, 2024 alipotembelea Mkoa wa Mbeya na kukutana na mwenyeji wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga na Maafisa wengine na kufanya mazungumzo.

Mkisi alipata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi ikiwemo Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania zamani CCP, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma.

 

Kamishna Mkisi ameendelea kuwajengea uwezo wa utendaji kazi Maafisa, Wakaguzi na Askari Polisi katika nyanja mbalimbali ili kuleta uweledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Kipolisi.

MRADI WA LTIP TUMAINI JIPYA LA KUINUA UCHUMI WA WILAYA YA MAKETE

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ni tumaini jipya la kuwainua kiuchumi wananchi wa wilaya ya Makete kwa ardhi yao kupangwa, kupimwa na kupata hati miliki ya ardhi ili kuendesha maisha yao ya kila siku kwa tija.

Lengo la kutekeleza mradi huo katika katika Halmashauri ya Makete na kusimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kutoa hati miliki za ardhi za kimila kwa wananchi wa halmashauri hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi ya Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Bw. William Makufwe hivi karibuni wakati anatoa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo wilayani hapo.

Friday, February 9, 2024

DC MALISA AWAKUMBUSHA MSD KUSIMAMIA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA KUKUSANYA MAPATO.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa imeitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Nyanda za Juu Kusini  kuvisimamia vituo vya kutoa huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya ikiwepo ununuzi wa bidhaa.

Malisa amesema leo Ijumaa Februari 9, 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau wa afya na watoa huduma mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Juma Homera.

Amesema Bohari ya Dawa Kanda ya Mbeya inatekeleza majukumu mawili ya kutunza na kusambaza bidhaa kwenye halmashauri 17 zenye vituo vya afya vya kutolea huduma za ya 884 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Makete Mkoa wa Njombe.

Thursday, February 8, 2024

CHAMA CHA MAPINDUZI KUJA NA MKAKATI MAALUMU WA KULIPENDEZESHA JIJI LA MBEYA.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema atazungumza na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani na Spika wa Bunge ili kuja mkakati wa kuzitengeneza barabara za mitaani, ili kulipendezesha jiji hilo.

Makonda ametoa kauli hiyo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Februari 7, 2024 katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Jijini Mbeya mara baada ya kutoridhishwa na majibu ya Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani humo, Albert Kindole kuhusu ujenzi wa barabara za mitaa ya Jiji hilo.

"Nitafanya mpango wa kuonana na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia, pia tutawasiliana na Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchangerwa) ili kuweka mkakati maalumu wa kulifanya Mbeya liwe jiji kweli kweli," amesema Makonda.

Awali akijibu swali la Makonda kuhusu mikakati ya ujenzi wa barabara, Meneja wa TARURA Kindole amesema barabara nyingi (takribani kilomita 18) za Jiji la Mbeya bajeti yake imeshatoka na wakandarasi wapo kazini, jambo lililoibua kelele za wananchi waliokuwa katika mkutano huo kuashiria bosi huyo haelezi ukweli.

Wednesday, February 7, 2024

SUMA JKT YAPATA TENDA YA UZOAJI TAKA KATA TANO ZA JIJI LA MBEYA

Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekabidhiwa magari 11 na Kampuni tanzu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Suma JKT kwa ajili ya kuanza mkataba wa  uondoshwaji wa taka katika kata tano.

Kampuni hiyo imepata  zabuni kati ya makampuni 16 yaliyojitokeza, huku ikieleza malengo yake ni  kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Mbeya inarejea katika nafasi ya kwanza kwa usafi katika Majiji kutoka nafasi ya mwisho.

Akizungumza na waandishi wa juzi baada ya kukabidhi magari hayo, Mkurugenzi mwendeshaji  kampuni ya usafi, Kepteni Rosemary Katani amesema wamejipanga kurejesha  hali ya usafi kwa Jiji la Mbeya.

“Tumejipanga kuhakikisha Jiji linarejea kwenye nafasi nzuri katika suala la usafi, kwa sasa tumekuja na vifaa vya kisasa na nguvu kazi kwa vijana 50 watakaofanya kazi usiku na mchana taka zote zinaondolewa kwa muda mfupi” amesema Nchimbi.

Friday, February 2, 2024

DC WA SONGWE ATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KIJIJI CHA NDANGA, AAGIZA WAHAME.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda ameagiza wananchi wa Kijiji cha Ndanga Kata ya Mbuyuni ambao nyumba zao zimeathiriwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha waondoke katika eneo huku akiutaka uongozi wa Kata hiyo kufanya tathimini na kusimamia zoezi la wananchi hao kuhama.

Itunda ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea eneo hilo ambapo, zaidi ya kaya 100 zimaathirika baada ya maji kujaa kwenye makazi yao na kuharibu nyumba na vitu mbalimbali.

“Baada ya kupata taarifa ya mafuriko kupitia diwani tumeamua kuja kujionea wenyewe. Viongozi tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi mahali salama lakini tuna jukumu kubwa kuwafariji wanapokutana na changamoto hii ya mafuriko’’ amesema Mkuu huyo wa Wilaya.