Sunday, December 31, 2023

AJALI YATOKEA SIMIKE: WATU KADHAA WAHOFIWA KUPOTEZA MAISHA.

Watu kadhaa wanahofiwa kufariki dunia katika ajali iliyotokea mapema leo Desemba 31, 2023 katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela kata ya Nzovwe Jijijini Mbeya.

Ajali hiyo imehusisha magari manne ikiwemo lori kubwa la mizigo, basi ndogo mbili za abiria (Toyota Hiace) ambazo zilikuwa na abiria zikifanya safari kati ya Mbalizi na Sokomatola pamoja na gari ndogo aina ya Toyota Sienta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Benjamin Kuzaga amekiri kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema kwa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa chanzo cha ajali ni Lori lenye namba za usajili T 428 DXD kufeli breki kisha kugonga gari nyingine tatu zikiwemo Toyota Hiace mbili zinazofanya safari kati ya Mbalizi na Sokomatola zilizokuwa na abiria ndani yake.

Friday, December 29, 2023

SPIKA WA BUNGE AINGILIA KATI SAKATA LA MGOGORO WA KANISA NA HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA.

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani ambae pia ni Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amelazimika kuingilia kati mgogoro wa Kanisa la The Children of Gospel for All International (TCH-GOLFN) na Halmashauri ya Jiji la Mbeya  unaohusisha uhalali wa umiliki wa eneo linalopaswa kujengwa kanisa na kuweka zuio kwa kipindi kirefu sasa.

Dkt. Tulia ambae pia ni Mbunge wa Mbeya mjini amefikia hatua hiyo baada ya kusikia uwepo wa mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya 20 ukihusisha Halmashauri ya Jiji na kusababisha waumini wa kanisa hilo kutaka kumuona Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati.

Akizungumza na waumini wa na Mchungaji wa kanisa hilo, John Ikowelo katika eneo lenye mgogoro Dkt. Tulia ametaka uongozi wa Jiji la Mbeya kupelekea nyaraka mbalimbali zinazoonyesha uhalali wa nani mmiliki wa eneo hilo.

Wednesday, December 27, 2023

POLISI MBEYA YAWAFUATA WATOTO KANISANI NA KUTOA ELIMU YA KUZUIA UHALIFU.

Wazazi, walezi na jamii yatakiwa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa malezi bora na elimu ya makuzi kwa watoto ili kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujithamini na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi yao.

Rai hiyo imetolewa Desemba 27, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga katika kongamano la watoto wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya linalofanyika katika Parokia ya Mwanjelwa Jijini Mbeya.

Kuzaga amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji na endapo wataona viashiria vya uhalifu huo watoe taarifa kwa viongozi wa dini na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Tuesday, December 26, 2023

TULIA TRUST YAGUSA WALEMAVU, WAZEE MAHITAJI YA CHAKULA NA KUBORESHA MAKAZI.

Taasisi ya Tulia Trust imekabidhi mahitaji ya chakula kwa wahitaji Wilayani Rungwe  kwaajili ya Sikukuu ya Krismasi.

Msaada huo uliokabidhiwa kwa kaya 13 ni pamoja na mchele, maharage na mafuta ya kula vyenye jumla ya thamani ya Sh. milioni 3.
Ofisa habari na Mawasiliano wa taasisi hiyo Joshua Mwakanolo amesema walengwa walionufaika ni ambao walibainika kwenye siku saba za kukimbiza bendera ya Upendo, Uwajibikaji na Mshikamano.

MABASI MATANO YAZUILIWA KUENDELEA NA SAFARI MBEYA KUTOKANA NA HITILAFU MBALIMBALI.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeyazuia mabasi matano ya abiria katika Stendi Kuu ya Mabasi Jijini Mbeya kuendelea na safari baada ya kukutwa na changamoto mbalimbali.

Akizungumza mapema leo Desemba 26, 2023 Mwanasheria Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Deus Sokoni baada ya kuendesha zoezi la ukaguzi wa Mabasi, Upimaji wa kilevi kwa madereva na utoaji wa elimu katika Stendi hiyo amesema jumla ya mabasi ya abiria 58 yamekaguliwa ambapo kati ya hayo mabasi matano kutoka kampeni ya TURU BEST, ISAMILO EXPRESS, ARUSHA EXPRESS, MSIGWA na AHMED yalikutwa na hitilafu katika mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa breki.

“Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama vile mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini (LATRA) limepewa mamlaka ya kuzuia chombo cha moto kuendelea na safari pindi linapofanya ukaguzi na kugundua changamoto ikiwemo ubovu na hitilafu katika mifumo ya chombo hicho” amesema Sokoni.

Sunday, December 24, 2023

DKT. TULIA AHAMASISHA WENYEVITI, MADIWANI KUELEZEA UTEKELEZAJI ILANI YA UCHAGUZI 2020.

Rais wa Mabunge Duniani ambae pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson amehamsisha Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za mitaa kwenda kufanya mikutano ya wananchi kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

Dkt. Tulia ambaye amesema hayo jana wakati akihutubia kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzo (CCM) Wilaya wenye  nia kuwahimiza upendo, umoja na mshikamano kwa lengo na  kukiimarisha chama kuelekea kwenye chaguzi mbalimbali.

Wednesday, December 20, 2023

MTANILA AMCOS CHUNYA KULIMA HEKTA 1,428 ZA TUMBAKU MSIMU WA 2024/2025.

Wakulima wa zao la Tumbaku Kata ya Lupa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya wanatarajia kulima hekta 1428 sawa na ekari 3,571 za zao hilo kwa msimu wa kilimo 2024/25.

Hatua hiyo itapelekea kuchuma kilo milioni 1.3 mpka milioni mbili za tumbaku ambazo zitauzwa kwenye masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku (Mtanila AMCOS) Isaya Hussein amesema kwenye Mkutano mkuu wa mwaka uliolenga kupitia taarifa za utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo katika umoja huo.

Saturday, December 16, 2023

KAMPENI YA 'AFYA CHECK' YAVUTIA VIJANA KUPIMA VVU KWA HIARI MKOANI MBEYA.

Kundi kubwa la vijana Mkoa wa Mbeya limejitokeza kwenye kampeni ya Afya Check kwa ajili ya kupima afya na kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU).

Kampeni hiyo yenye lengo la kuhamasisha vijana kwenye vyuo vya elimu ya juu 9 na kufikia vijana 4,000 Jijini Mbeya kwa ufadhiri wa Shirika la HJMRI ambayo inaendeshwa kwa makundi mbalimbali mkoani hapa.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia kundi kubwa la vijana kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU huku kati ya kundi la watu 10 mmoja hukutwa na maambukizi sambamba na Mkoa kushika nafasi 2 kitaifa kwa kuwa na asilimia 9.3.

Thursday, December 14, 2023

TULIA TRUST YAHITIMISHA ZOEZI LA KUPEPERUSHA BENDERA YA UPENDO.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust Joshua Mwakanolo (kulia) akikabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya wodi ya mama na mtoto katika Hosptali ya Makandana Wilaya ya Rungwe Mkoa Mbeya jana Alhamisi Desemba 13, 2023.

Taasisi ya Tulia Trust jana imehitimisha zoezi la kupeperusha bendera yenye ujumbe maalum wa Upendo, Uwajibikaji kwa jamii Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya ambayo ilianza kupeperushwa Desemba 9 mwaka huu.

Ofisa Habari na Mawasiliano, Joshua Mwakanolo amesema leo wilayani humo wakati akikabidhi mahitaji mbalimbali kwa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya  Wilaya ya Makandana.

Tuesday, December 12, 2023

WANANCHI WAOMBA KUAZISHWA KWA HALMASHAURI MPYA MAKETE, NJOMBE.

Wananchi na wadau wa maendeleo wa kata 11 kati ya 23 za halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe wameiomba serikali kuigawa halmashauri hiyo na kuazisha halmashauri mpya kutokana na jiografia ya wilaya hiyo.
 

Kikao cha kupata maoni ya wadau mbalimbali juu ya kupata halmashauri mpya ya wilaya ambayo wamependekeza kuipa jina la halmashauri ya wilaya kitulo ni kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma kutokana na umbali kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya mama ya Makete.

 

Wananchi wameiomba selikali kuwepo na halmashauri mbili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo vyeti ya kuzaliwa, vitambulisho vya NIDA, huduma benki na huduma nyingine za kijamii.

 

Mwenyekiti wa kikao hicho Bi. Rhoda Nsemwa ameiambia Mwananchi kuwa wananchi wasihofu kuhusu vigezo kwa kuwa serikali inaangalia mambo mengi hadi kufikia hatua ya kugawa eneo la kiutawala na kuwa halmashauri ya wilaya.

Monday, December 11, 2023

ZAIDI YA WATU 233,000 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI WA MUGANGO KIABAKARI, BUTIAMA

Naibu wa Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka wakandarasi wa mradi wa maji wa Mugango - Kiabakari - Butiama waweze kukamilisha utekelezaji wa Ujenzi wa mradi huo ili wananchi zaidi ya laki 233,000 waweze kunufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mhandisi Mahundi ameyasema hayo Desemba 11, 2023 Wilayani Butiama Mkoani Mara wakati wa ziara yake ya  kukagua utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa maji wa Mugango Kiabakari na Mradi wa Maji wa Kijiji cha Kyankoma Kiagata.

Sunday, December 10, 2023

TULIA TRUST YAKABIDHI KITI MWENDO KWA MLEMAVU ALIYESOTA MIAKA SABA RUNGWE.

Taasisi ya Tulia Trust imekabidhi kiti mwendo kwa mtoto Ester Seme (7) mkazi wa kijiji cha Ilolo Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya alipata ulemavu tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja mara baada ya kumpoteza mama yake mzazi.

Kiti hicho kimekabidhiwa jana na Ofisa Uhusiano na Mawasiliano, Joshua Mwakanolo  kwa bibi wa mlemavu huyo Justina Seme (80) kwa lengo la kumsaidia kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Pia Mwakanolo alikabidhi  bendera yenye ujumbe maalum wa uwajibikaji, upendo na ushirikishwaji kwa jamii ikiwa ni maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi kitimwendo, Mwakanolo amesema kitendo hicho ni kuikumbusha jamii kurejea kwenye dhana ya uwajibikaji, upendo, mshikamano na ushirikiano.

Saturday, December 9, 2023

SAA TISA BARABARA YA MBEYA - TUNDUMA YAFUNGWA, WANANCHI WALILIA NJIA NNE.

Shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo zimekwama kwa zaidi ya saa tisa katika eneo la Simike barabara kuu ya Mbeya - Tuduma baada ya gari la mizigo kuanguka na kuziba njia.

Ajali hiyo imesababisha kuziba njia na kufanya shughuli za usafiri na usafirishaji kwenda mikoa na nchi jirani kusimama tangu saa 3:30 - hadi saa 12:00 baada gari hilo kuvutwa.

Lugano Asumwisye mkazi wa Uyole ameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya njia nne kwani ufinyu wa barabara imekua kero na kukwamisha shughuli za kiuchumi na kupoteza mapato ya serikali.

"Ni muda sasa tunasikia ujenzi wa njia nne utaanza ila tunaona hatua zinazochukuliwa zinaenda taratibu sana, serikali iliangalie hili kwa umuhimu wake linakwamisha mambo mengi, tangu saa tatu nipo hapa ningekua nimeshafika Tunduma na kuendelea na shughuli zangu".

Serikali inakusudia kujenga barabara ya njia nne itakayosaidia kupunguza msongamano wa magari kutoka Nsalaga hadi Ifisi (Km 29) barabara itayogharimu Bilioni 138.7.

VICOBA KUWAKOMBOA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA.

 
Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo amepongeza kitendo cha baadhi klabu za waandishi wa habari nchini kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA).

Akiongea mara baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya klabu hizo yaliyofanyika Desemba 09, 2023 katika viunga vya ofisi ya UTPC Nsokolo amesema kuanzishwa kwa VICOBA kutasaidia waandishi kuendelea kutimiza wajibu wao  wa kuitumikia jamii mbali na kucheleweshwa kwa kupata stahiki zao.

Friday, December 8, 2023

MAADHIMISHO YA MIAKA 62 YA UHURU WA TANGANYIKA.

Kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe inakusudia kuadhimisha siku hiyo kwa namna tofauti kwa kufanya usafi wa mazingira, upandaji miti na michezo mbalimbali.

Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffary Haniu amewahamasisha wananchi kushiriki shughuli za usafi, upandaji miti na michezo mbalimbali sambamba na kudumisha amani na utulivu iliyoachwa na waasisi wa Taifa letu.

Maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Tandale Tukuyu Mjini ambapo pamoja na mambo mengine itashuhudiwa michezo mbalimbali ikifanyika.

Kauli mbiu katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni "Umoja na mshikamano ni chachu ya maendeleo ya Taifa letu".

Wednesday, December 6, 2023

CHUTCU WACHANGIA VITANDA NA MASHUKA KITUO CHA AFYA LUPA WILAYANI CHUNYA.

Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya Chunya (CHUTCU) kimechangia  vitanda vitatu kikiwepo cha kujifungulia akina mama wajawazito na mashuka 20 kwa lengo la kuboresha kupunguza changamoto katika Kituo cha Afya Lupa.

Meneja Mkuu wa CHUTCU, Christian Msigwa amekabidhi msaada huo jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka Saimon katika hafla fupi iliyofanyika katika Kituo hicho cha afya.

“Miongoni mwa vitu tulivyokabidhi ni pamoja na vitanda vitatu, kimoja cha kujifungulia,  uchunguzi, taa maalum na mashuka 20 vyote vikiwa na thamani ya Sh 4 million” amesema Msigwa.

Tuesday, December 5, 2023

DC HANIU AZINDUA ZOEZI LA UGAWAJI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA).


Mkuu wa wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu amezindua zoezi la ugawaji wa Vitambulisho Taifa (NIDA) leo Desemba 5, 2023.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Kyimo wilayani humo, Haniu ameeleza kuwa jumla ya vitambulisho 69638 vitatolewa  kwa Wakazi wa wilaya ya Rungwe huku Kata ya Kyimo ikipokea jumla ya vitambulisho 2850.

JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA LAMSHUKURU IGP KWA KUWAONGEZEA VITENDEA KAZI.

Wakaguzi wa Kata nane Mkoani Mbeya wamekabidhiwa pikipiki aina ya Boxer kwa ajili ya kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao katika Kata hizo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya pikipiki hizo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura kwa kutambua umuhimu wa vitendea kazi katika kufanikisha utekelezaji wa kazi mbalimbali kwa wakaguzi wa Kata.

Saturday, December 2, 2023

WANANCHI WATAKIWA KUACHA UTAMADUNI WA KUHIFADHI MAJUMBANI MIILI YA NDUGU ZAO WALIOFARIKI.

Wananchi Wilayani Mbarali wametakiwa kuacha utamaduni wa kuhifadhi majumbani miili ya wapendwa wao waliopoteza maisha na badala yake wawapeleke katika vituo vya kutokelea huduma za afya kwani serikali imeboresha huduma za afya ikiwemo vyumba vya kuifadhia maiti.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Dkt. Ray Salandi mbele ya kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ilipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika sekta ya elimu na afya ukiwemo mradi wa jengo la kuhifadhi maiti ‘mochwari’ katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali.

Dkt. Salandi amesema serikali imenunua mashine nyingi za kuhifidhia maiti akivitaja vituo vya afya vya Madibila, Utengule Usangu na Rujewa kuwa kila kimoja kina mashine yenye uwezo wa kuhifadhi maiti tatu huku Hospital ya Wilaya ikiwa na mashine ya kuhifadhi miili kumi na mbili kwa wakati mmoja hivyo kama wilaya ina nafasi za kuhifadhi Maiti 21.

Friday, December 1, 2023

DC RUNGWE AKEMEA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO.

Jaffary Haniu, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffary Haniu amekemea vitendo vya ukatili kwa watoto na jamii kwa ujumla ambavyo kwa namna moja au nyingine vinachangia kuongezeka kwa maambukizi ya UKIMWI.

Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kwa Mkoa ya Mbeya yamefanyika Wilayani Rungwe, Haniu ametaja vitendo ukatili kuwa ni pamoja na ubakaji ulawiti na ukeketaji katika baadhi ya  mikoa nchini Tanzania.

Haniu amehamasisha wananchi kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya maendeleo.

Thursday, November 30, 2023

HALMASHAURI YA WILAYA YA RUNGWE KUJENGA MAEGESHO YA BODABODA


Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Renatus Mchau ameahidi kujenga vituo vya maegesho ya bodaboda katika mji wa Tukuyu na vitongoji vyake ikiwa ni jitihada ya kuboresha mazingira ya usafirishaji wa abiria na mali zao.

Ahadi hii ameitoa katika kikao maalumu cha viongozi wa Bodaboda ambapo pamoja na viongozi wengine pia Kikosi cha Usalama Barabarani kutoka jeshi la polisi kimeshiriki.

Thursday, November 16, 2023

WAWEKAZAJI WA UTALII MKOA WA TANGA WATAKIWA KUJIANDAA NA MKUTANO WA WADAU WA MAZAO YA NYUKI DUNIANI 2027.

Wadau wa sekta ya utalii, sekta ya ufugaji nyuki na mazao yatokanayo na Nyuki wametakiwa kujiandaa na mkutano mkubwa wa wadau wa ufugaji nyuki na wazalishaji wa mazao yatokanayo na ufugaji nyuki utakao fanyika Jijiji Arusha mwaka 2027.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amesema hayo alipokuwa anatoa salamu za Wizara kwenye Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii na Uzinduzi wa Mwongozo wa uwekezaji Mkoa wa Tanga.

Mh. Kitandula alisema kwamba kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa katika kongamano na maonesho yanayoendelea katika mabanda, anaamini kuwa wawekezaji wengi watavutiwa kuja kuwekeza katika Mkoa wa Tanga kwani fursa nyingi zitaelezwa hapa zikiwemo za sekta ya Utalii.

 

Monday, May 8, 2023

WIZARA YA KILIMO YATENGA BIL. 970

 

Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Mohammed Bashe (Mb)

Wizara ya Kilimo leo imeomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi 970,785,619,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha 2023/ 2024.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni mjini Dodoma leo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, utekelezaji wa Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2023/2024 umejikita katika maeneo matano ya kipaumbele na mikakati ya utekelezaji 26.

“Shughuli za kilimo hapa nchini ni muhimu kwa maisha na ustawi wa watu na uchumi wetu. Kimsingi, kilimo ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini wa kipato na umaskini wa chakula.

“Kilimo kinapanua fursa za ajira kwa kushirikisha wananchi wengi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na hususan biashara ya mazao ya kilimo ndani ya nchi na kimataifa,” amesema Waziri Bashe.