Rais wa Mabunge Duniani ambae pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson amehamsisha Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za mitaa kwenda kufanya mikutano ya wananchi kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Dkt. Tulia ambaye amesema hayo jana wakati akihutubia kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzo (CCM) Wilaya wenye nia kuwahimiza upendo, umoja na mshikamano kwa lengo na kukiimarisha chama kuelekea kwenye chaguzi mbalimbali.
Amesema serikali imetekeleza miradi mbalimbali nchini na Jijini Mbeya licha ya miradi ya elimu na afya lakini Jiji la Mbeya limepata mradi mkubwa wa barabara ya njia nne na mradi wa maji wa Kiwira.Aidha amewataka wajumbe kulinda viti vyote vya CCM kuanzia ngazi ya Mtaa, Diwani, Mbunge na Rais kwani itakuwa ni aibu na ni vema kila mmoja akawaeleza wananchi namna chama kilivyoisimamia serikali kikamilifu.
"Huu si muda wa kupigana vijembe ingawa kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote lakini kwa sasa tuwaache waliopo watekeleze majukumu yao" alisema Dkt. Tulia.
Hata hivyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoelekeza miradi mkoani Mbeya hivyo ni vema kila mmoja anampa kura za kishindo kipindi cha uchaguzi mwaka 2025.
Pia ameagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha wanapaua maboma ya vyumba vya madarasa na zahanati ili wananchi wapate huduma bila vikwazo.
Amesema hakuna mwanafunzi atayekosa dawati mara shule zitakapofunguliwa mapema mwaka 2024 kwani mipango yote ipo vizuri hivyo wazazi wawahimize watoto kusoma.
Naye Diwani wa viti maalum Kata ya Isanga, Atupele Msai amesema wanakwenda kutekeleza maagizo ya Mbunge wa Mbeya mjini, Dkt. Tulia Ackson kueleza miradi iliyoelekezwa na Serikali.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru, Mbunge wetu, Spika na Rais wa Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson kwani uwepo wake umeleta miradi mingi ya maendeleo ya wananchi ikiwepo elimu, afya, maji na barabara” amesema Msai.
No comments:
Post a Comment