Wazazi, walezi na jamii yatakiwa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa malezi bora na elimu ya makuzi kwa watoto ili kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujithamini na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi yao.
Rai hiyo imetolewa Desemba 27, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga katika kongamano la watoto wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya linalofanyika katika Parokia ya Mwanjelwa Jijini Mbeya.
Kuzaga amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji na endapo wataona viashiria vya uhalifu huo watoe taarifa kwa viongozi wa dini na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Pia Kuzaga ameeleza kuwa, mbali na elimu ya ukatili wa kijinsia, watoto hao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya vivuko vya watembea kwa miguu (Zebra Crossing) pamoja na matumizi sahihi ya taa za kuongozea magari hasa pindi wanapotaka kuvuka Barabara.
Naye, Mkurugenzi wa mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, shirika linalojihusisha na utoaji wa elimu ya malezi na makuzi kwa watoto, Padri Richard Mgasa amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwajengea uwezo wa watoto katika masuala ya kidini, kujua haki zao, kujitambua na kujilinda dhidi ya vitendo viovu.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya Mratibu Msaidizi wa Polisi Veronica Ponela ametoa wito kwa wazazi na jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake watoe taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi ili hatua zichukuliwe.
Jeshi la Polisi nchini limeendelea kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii kwa lengo la kutoa elimu na kuwajengea uwezo katika masuala ya kiusalama na kujua haki na wajibu wao ikiwemo kushirikiana kuzuia uhalifu na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
No comments:
Post a Comment