Wednesday, December 6, 2023

CHUTCU WACHANGIA VITANDA NA MASHUKA KITUO CHA AFYA LUPA WILAYANI CHUNYA.

Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya Chunya (CHUTCU) kimechangia  vitanda vitatu kikiwepo cha kujifungulia akina mama wajawazito na mashuka 20 kwa lengo la kuboresha kupunguza changamoto katika Kituo cha Afya Lupa.

Meneja Mkuu wa CHUTCU, Christian Msigwa amekabidhi msaada huo jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka Saimon katika hafla fupi iliyofanyika katika Kituo hicho cha afya.

“Miongoni mwa vitu tulivyokabidhi ni pamoja na vitanda vitatu, kimoja cha kujifungulia,  uchunguzi, taa maalum na mashuka 20 vyote vikiwa na thamani ya Sh 4 million” amesema Msigwa.
Msigwa amesema msaada huo ni takwa la kisheria kwa vyama vikuu na AMCOS  kuchangia huduma za kijamii na kwamba huo ni mwanzo wataendelea kugusa maeneo mengine yenye uhitaji.

“Tumeona ni vyama sasa kurejea kuleta mchango wetu kwenye jamii, ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto wakati wa kujifungua lengo ni kuunga mkono jitihada za Serikali kusaidia sekta ya afya na  kupuguza changamoto za masuala ya uzazi” amesema Msigwa.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Kaimu Mganga mfawidhi, Dkt. Obeid Prosper amesema vitanda hivyo vitapunguza changamoto iliyopo hususan kwa wajawazito wanapofikia wakati wa kujifungua  kwani kuna uhitaji wa vitanda 10 vilivyopo viwili.

Amesema idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa wakinamama wajawazito wanaofika kujifungua kwa wiki wakiwa sita mpaka saba huku kwa mwezi wakiwa 137.

“Unaona hapo uwiano haupo sawa idadi ya wagonjwa ni kubwa kuliko idadi ya vitanda kwani kuna wakati tunazidiwa na kulazimika kutumia vitanda vya wagonjwa wa kawaida kwa ajili ya kujifungulia wajawazito ”amesema Prosper.

Amesema mbali na changamoto ya vitanda pia kuna tatizo la kukosekana kwa huduma ya maji jambo ambalo linapelekea ndugu wa wagonjwa kutembea umbali mrefu kufuatia huduma ikiwepo kufua nguo za wagonjwa kwa kila kilichoelezwa uwepo wa mashine ambayo imeshindwa kutumika kutokana na ukosefu wa maji ya uhakika.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya Saimon Mayeka Saimon ameshukuru Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku (CHUTCU) kwa kujitoa kusaidia kuchangia sekta ya afya na kwamba ni thawabu mbele za Mungu.

“Hili mlilofanya mtapata thawabu kubwa mbele za Mungu niwatake tu kuendelea kushirikiana na Serikali kuchangia jamii ikiwa ni takwa la kisheria kwa vyama za msingi Amcos nchini ” amesema Mayeka.

Nae mama mjamzito, Stella Amos amesema msaada huo utakuwa mwarobaini wa kuondokana na changamoto ya utoaji huduma za kujifungua kwa wakinamama wajawazito katika Kituo cha afya Lupa.

No comments:

Post a Comment