Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Mohammed Bashe (Mb)
Wizara ya Kilimo leo imeomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi 970,785,619,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha 2023/ 2024.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni mjini Dodoma leo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, utekelezaji wa Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2023/2024 umejikita katika maeneo matano ya kipaumbele na mikakati ya utekelezaji 26.
“Shughuli za kilimo hapa nchini ni muhimu kwa maisha na ustawi wa watu na uchumi wetu. Kimsingi, kilimo ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini wa kipato na umaskini wa chakula.
“Kilimo kinapanua fursa za ajira kwa kushirikisha wananchi wengi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na hususan biashara ya mazao ya kilimo ndani ya nchi na kimataifa,” amesema Waziri Bashe.
Amesema Taifa lolote duniani usalama wa kwanza wa nchi ni kujitosheleza kwa chakula, hakuna maendeleo ya kweli kama hakuna chakula, lakini hakuna chakula kama hakuna wakulima.
“Mimi na Wizara ninayoiongoza nitaendelea kulinda maslahi ya wakulima na wadau wa sekta ya kilimo. Hivyo, ninawaomba kwa heshima na taadhima waheshimiwa Wabunge muiunge mkono Serikali katika mageuzi haya ya muda mrefu.
“Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 970,785,619,000 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 ikiwa ni ongezeko la asilimia 29.24 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2022/2023,” amesema.
Credit: Habari Leo.
No comments:
Post a Comment